Mahakimu kitanzini


* Watakaotuhumiwa rushwa kufutwa kazi
* Haijalishi wameshinda au kushindwa kesi

Mary Kitosio, Arusha

Jaji Mkuu Mohamed Chande
JAJI Mkuu wa Tanzania, Mohamed Chande, ameshauri mahakimu watakaoshitakiwa kwa rushwa waondolewe kazini.

Akizungumza na majaji wafawidhi wa Mahakama Kuu na wengine jijini hapa jana, Jaji Mkuu Chande alitoa ushauri huo kwa Tume ya Utumishi wa Mahakama, akiwataka mahakimu kusimamia maadili na atakayebainika amepokea rushwa ataondolewa kazini.

Alisema idara nyingi za Mahakama zinaonekana kulalamikiwa na wananchi kwa rushwa na watakaobainika hatua kali zitachukuliwa dhidi yao.

“Mahakimu wa ngazi za chini wamekuwa wakilalamikiwa na wananchi kwa kutosimamia maadili, nimeshatoa ushauri kwa Tume, kwamba hakimu atakayeshitakiwa kwa rushwa ataondolewa kazini hata kama atashinda kesi,” alionya Jaji Mkuu Chande.

Jaji Mkuu pia aliwataka majaji kuja na mikakati ya kuhakikisha kasi ya kupunguza kesi mahakamani inaongezeka hasa za muda mrefu ili kupunguza malalamiko yanayotokana na kuchelewa kutoa hukumu na kutopatikana kwa nakala za hukumu kwa wakati.

Pia Jaji Mkuu aliwataka majaji kusimamia maadili ndani ya taasisi hiyo ili kurejesha imani ya wananchi kwa Mahakama yao.

Katika hatua nyingine, Jaji Mkuu aliwapongeza majaji na majaji wafawidhi kwa kumaliza vizuri kesi za uchaguzi zilizofunguliwa kwenye Mahakama Kuu nchini pamoja na kutenga muda wa kujadili changamoto zilizotokana na kesi hizo.

Alisema majaji hao walijitolea kusikiliza kesi hizo na nyingi kuzitolea hukumu kwa kipindi kifupi licha ya chache kubaki mahakamani.

Kwa mujibu wa Jaji Mkuu Chande, jumla ya kesi 53 za ubunge zilizotokana na Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana zilifunguliwa Mahakama Kuu kanda za Dar es Salaam, Dodoma, Iringa, Mbeya, Moshi, Mtwara na Mwanza.

Kanda nyingine ni Shinyanga, Songea, Sumbawanga na Tanga ambapo kati ya hizo, 31 zilimalizika katika hatua za awali na 22 ziliendelea na hadi sasa 19 zimemalizika na tatu bado ziko mahakamani.

Hata hivyo, kesi zote 196 zilizotokana na uchaguzi wa madiwani zilimalizika mapema katika mahakama mbalimbali za mahakimu wakazi nchini katika kipindi cha mwaka mmoja tangu kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu.

Zaidi ya asilimia 94 ya kesi za uchaguzi zilizofunguliwa kwenye Mahakama Kuu zimemalizika wakati asilimia 100 ya kesi zote za udiwani zimemalizika pia.

Katika mkutano huo, Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu, Ferdinand Wambali alisema Watanzania wana imani na Mahakama, hivyo ni muhimu majaji na mahakimu wakatenda haki kwa wote na wakati wote.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo