Serikali yakwama kwenye mashambapori


Joyce Kasiki, Dodoma

SERIKALI inashindwa kuyafutia hatimiliki mashambapori mengi ambayo hayajaendelezwa baada ya kubaini kuwa yamekopewa mabilioni ya fedha kutoka taasisi za kibenki hapa nchini.

Hata hivyo, imezihadharisha taasisi za kibenki kuwa makini kwani endapo zitatoa mikopo kwa dhamana ya mashamba na yakaleta migogoro kwa kutoendelezwa, itazishughulikia.

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi aliitoa kauli hiyo mjini  hapa jana mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, wakati akijibu hoja za wabunge baada ya Serikali  kuwasilisha taarifa ya  ardhi kuhusu hatima ya matumizi ya mashamba makubwa yaliyotelekezwa.

Hata hivyo, alisema ni jukumu la Serikali kulinda umiliki halali kwa watu wenye hatimiliki badala ya kuwanyang’anya mashamba kiholela.

“Rais ametupa jukumu la kuhakikisha tunafuta  mashamba yasiyoendelezwa, na kazi hiyo inaendelea, lakini tunafuata  sheria ili tusijeshitakiwa," alisema Lukuvi.

Alisema wakati wakiendelea na utaratibu wa kufuta mashamba yasiyoendelezwa, walibaini kuwapo mengi yenye mikopo kutoka taasisi za kibenki na hivyo lazima wafuate taratibu ili benki zisifilisiwe.

Waziri huyo alisema katika mashamba hayo kuna yaliyochukuliwa mikopo nje na ndani ya nchi na orodha yote wanayo na wanaendelea kuifanyia kazi kikamilifu.

Alisema wakati taasisi za kibenki zikijigamba kushiriki katika sekta ya kilimo, zimekuwa zikishindwa kuangalia uhalisia ikiwa ni pamoja na kufika kwenye mashamba husika kuona kama yanaendelezwa.

"Mkakati wa wizara yangu hivi sasa, ni kukutana na taasisi za kibenki zote ambazo mashamba hayo yamekopea, ili tuweze kufanya mazungumzo na kuona namna bora ya kumaliza mgogoro huo,” alisema.

Alitolea mfano wa shamba lililokopewa dola milioni 16 za Marekani mara nane, na hivyo kusababisha ugumu wa kazi hiyo.

Lukuvi alisema kwa bahati mbaya licha ya mikopo hiyo kukopwa kwa dhamana ya mashamba lakini haitumiki kuwekeza kwenye mashamba bali kwenye biashara nyingine ikiwamo kujenga nyumba za kupangisha nje ya nchi.

Alisema, endapo ingekuwa fedha hizo zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa, sekta ya kilimo nchini ingekuwa na mafanikio makubwa.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo