Mufti kuongeza muda wa Tume


Salha Mohamed

Shekhe Abubakar Zubeir
MUFTI Mkuu wa Tanzania, Shekhe Abubakar Zubeir, amesema huenda muda wa Tume aliyounda kuchunguza mali za Waislamu nchini ukaongezwa.

Tume hiyo iliyoundwa Agosti 10 yenye wajumbe wanane ilitokana na agizo la Rais John Magufuli Julai 6 kwenye Baraza la Iddi akitaka kuunda timu ya kufuatilia kadhia ya mali za Waislamu zilizo chini ya Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata).

Akizungumza jana na JAMBO LEO, Shekhe Zubeir alisema bado Tume haijamaliza uchunguzi na ikimaliza wautaweka wazi.

“Bado Tume inaendelea, bado muda na ukiangalia kazi ya kuchunguza si ndogo ni kubwa na huenda tukawaongeza muda wa kazi hiyo,” alisema.

Alisema kulingana na kazi inayofanya Tume hiyo, si ya   siku mbili au tatu, hivyo inahitaji muda hasa ikizingatiwa kuwa inazunguka nchi nzima.

Alisema mbali na Tume hiyo kufuatilia nchi nzima kwa kutembelea sehemu husika, hivyo jamii inapaswa kuiombea imalize kwa mafanikio.

Mwezi jana, Makamu Mwenyekiti wa Tume hiyo, Shekhe Issa Issa aliwataka wananchi wenye taarifa za mali za Waislamu zilizo chini ya usimamizi na umiliki wa Bakwata, kuwasilisha kwenye Tume.

"Mwenye taarifa zozote za nyaraka au wenye taarifa za ushahidi wowote wa ubadhirifu wa mali za Waislamu zilizo chini ya usimamizi na umiliki wa Bakwata awasilianena Tume ya Mufti," alisema.

Alisema katika kufanikisha jukumu hilo, Tume inafanya kazi kwa kushirikiana na wataalamu na vyombo   mbalimbali kufanikisha jukumu hilo huku akiahidi na kuhakikishia Waislamu na Watanzania kuwa Tume hiyo ni huru inafanya kazi zake bila kuingiliwa na mtu au chombo chochote.

Alisema itafuatilia misamaha ya kodi zilizoombwa na Baraza na taasisi zake nchi nzima, mikataba yote ya uuzaji wa viwanja na mali za Baraza na taasisi zake nchi nzima, kuona uhalali wa umiliki huo.

Pia alisema itafuatilia mikataba yote ambayo Baraza na taasisi zake zilizoingia na wawekezaji na kuona mikataba hiyo kama ina maslahi kwa Baraza na taasisi zake, lakini pia kuona hali ya usajili wa mali hizo.

"Pia Tume itafuatilia mapato na matumizi ya Baraza na taasisi zake na kupeleka taarifa na mapendekezo hayo kwa Mufti ndani ya siku 90," alisema.

Aliongeza kuwa baada ya kumaliza kukusanya taarifa hizo wataziwasilisha kwa Mufti na ofisi yake itaweka  hadharani taarifa hiyo ikiwa ni pamoja na kuchukuliwa hatua stahiki.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo