Watoto 138 kufanyiwa upasuaji wa moyo mwezi huu


Salha Mohamed

TAASISI ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), imepokea msaada wa Sh. milioni 303 kwa ajili ya upasuaji wa watoto 138 wenye matatizo ya moyo nchini.

Fedha hizo zilizotolewa na taasisi za I & M Bank, Baps Charities na Youth walfare Trust, zitasaidia kupunguza gharama za upasuaji kwa watoto hao iwapo wagepata huduma hiyo nje ya nchi.

Mkurugenzi Mkuu wa JKCI, Profesa Mohamed Janabi alisema kabla ya Novemba watakuwa wamefanya upasuaji kwa watoto hao ili kuokoa maisha yao huku akizitaka taasisi zingine kujitokeza kusaidia.

“Awamu ya kwanza ilikuwa na wagonjwa watoto 500 huku  wengine 211 wakiwa ni watu wazima. Tayari tumehudumia wagonjwa wa moyo 728 katika kipindi cha miezi tisa cha Januari hadi Septemba mwaka huu,” alisema Profesa Janabi.

Alisema wagonjwa hao kama wangepatiwa huduma hiyo nje ya nchi, wangetumia sh. milioni 23 kila mmoja na kwamba huenda wengine wangefariki kutokana na kushindwa kwenda kutibiwa.

“Tumefanya upasuaji lakini fedha tunazopata hazikamilishi gharama zote, bali imesaidia kwa kiasi kikubwa kununua vifaa vya upasuaji,”alisema.

Mkurugenzi wa Utafiti JKCI, Dk Pedro Pallangyo alisema mwaka jana walitoa huduma ya Cath Lab(upasuaji bila kupasua kifua) kwa wagonjwa 234 ambapo kwa mwaka huu Januari hadi Septemba walitoa huduma kwa wagonjwa 494.

“Hii ni zaidi ya mara nne ya tuliyofanya mwaka jana,  kwa huduma ya kupasua kifua mwaka jana tulihudumia wagonjwa 204 mwaka huu miezi 9 ya kwanza tumehudumia wagonjwa 234 sawa na ongezeko la asilimia 116 ukilinganisha na mwaka jana,”alisema.

Alishukuru Taasisi ya I&M Bank kwa kutoa Sh milioni 33 zitakazo saidia kufanya upasuaji kwa watoto 15, Taasisi ya Youth Walfare Trust iliyotoa Sh milioni 48.4 zitakazosaidia upasuaji kwa watoto 22.

Pia aliipongeza taasisi ya Baps Charity kwa kutoa Sh milioni 222 kwa ajili ya upasuaji wa watoto 101, huku taasisi hiyo ikifanya muendelezo wa kile ambacho walifanya awali kwa kutoa kiasi kama hicho na kufanyiwa upasuaji watoto 100.

Alisema kama idadi ya wagonjwa waliopimwa magonjwa ya moyo na kuhitaji kufayiwa upasuaji hawataongezeka zitahitajika zaidi ya Sh milioni 800 kufaya upasuaji wa moyo na kubainisha kuwa uhitaji utakuwepo kwani magonjwa hayo hayajaisha.

Mama mzazi wa Mtoto John Mayatab mwenye umri wa miezi nane, anayesumbuliwa na matatizo zaidi ya manne kwenye moyo, Neema Daudi alisema tatizo la mtoto wake liligundulika akiwa na mwezi mmoja, ambapo alikuwa anashindwa kunyonya huku akitokwa na jasho hata kama hakuna joto, hivyo aliitaka jamii kupima afya za watoto wao.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo