Uchaguzi: 'Mdudu' anayeitafuna Afrika


UCHAMBUZI HURU

Mashaka Mgeta

Mashaka Mgeta
DUNIANI hakuna nchi inayoweza kufanya chaguzi zake pasipo malumbano miongoni mwa wagombea, wanachama ama wafuasi wa vyama vinavyoshiriki. Hali hiyo inatokea katika nchi za Afrika, Asia, Pacific, Ulaya na kwingineko duniani.

Kuna tofauti ya namna malumbano yanavyotokea, vyanzo na mfumo thabiti ya utatuzi wake.

Kwa sehemu kubwa, nchi kadhaa hususani zilizoendelea na chache kati ya zinazoendelea, zimefanikiwa kuendesha chaguzi zao kwa kufuata mfumo chanya, ambao malumbano na mbinu zinazotumika kupata ushindi, haviathiri umoja wa taifa husika.

Kwa bahati mbaya, nchi nyingi za Afrika iliyowahi kuitwa ‘bara la giza’, na pengine kutokana na matendo ya baadhi ya watawala wake, inaweza kustahili kuitwa hivyo hali inazidi kuwa mbaya.

Malumbano na mbinu zinazohusiana na uchaguzi vimekuwa sababu ya machafuko, kutoweka kwa umoja wa kitaifa na wakati mwingine vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Mifumo ya chaguzi nyingi katika Afrika ni mizuri kutokana na sababu kadhaa, ikiwamo ushirikishi mpana wa wananchi kuwachagua viongozi katika ngazi za tawala za mikoa na serikali za mitaa.

Lakini utekelezaji hasi wa sheria za uchaguzi ili kulinda maslahi ya kisiasa hasa kwa watawala, matumizi ya nguvu kubwa katika kuutafuta na ‘kuumiliki’ ushindi na rushwa, vinachangia kuzivuruga jamii za Afrika, hivyo kuzidisha wigo wa mafarakano.

Jamii zinazofarakana haziwezi kushiriki katika ubunifu bora wa miradi, mikakati na mipango ya kuwaondoa watu katika umasikini.

Kwa mafarakano yanayotokana na chaguzi barani Afrika, jamii zinaendelea kuishi kimasikini, kuendeleza ujinga na kushindwa kuyadhibiti maradhi kwa kadri ilivyokuwa kusudio la kumuondoa mkoloni.

Tawala nyingi za Afrika zinashutumiwa kwa kukiuka sheria na kanuni za uchaguzi, kisha kutumia dola kuwadhibiti wanaotafuta haki na usawa kwa maslahi ya umma mpana.

Kwa namna hiyo, miongoni mwa malengo ya kuwaondoa wakoloni na kuifanya Afrika kuwa huru, hayajafikiwa na huenda yakachukua muda mrefu kufikiwa kutokana na ukiukwaji wa sheria na kanuni za chaguzi.

Chaguzi zinapohujumiwa, michakato yake ‘ikachakachuliwa’ ikiwa ni sehemu ya jitihada za kutafuta na kumiliki utawala, mataifa yakabaki katika mafarakano ya ndani, wanavurugana wenyewe kwa wenyewe.

Wanaoratibu mbinu zinazoathiri mchakato wa chaguzi, wamekuwa wakitumia ‘nyenzo’ kama vyombo vya dola, mamlaka za kusimamia uchaguzi husika na rushwa hasa ya vyeo, ili kufanikisha nia ya kupata ushindi.

Matukio hayo yanatumika kwa kizazi kilichopo na kinachokuja. Tangu kuondoka kwa waasisi wa uhuru wa mataifa mbalimbali Afrika, waliowafuata, kidogokidogo, wakaanza kushiriki njama na mbinu chafu zinazowatenganisha na kuwafarakanisha raia wao.

Wenye mamlaka wanawateuwa wasaidizi wao wakiwamo wa mamlaka za kusimamia uchaguzi ama taasisi kama mahakama za Katiba, ili kuhalalisha `uovu’ unaowaweka madarakani.

Jambo lililo dhahiri ni kwamba mbinu hizo zinafanikiwa katika maeneo mengi ya Afrika.

Watawala wanaendelea kubaki madarakani, wakimiliki dola na tawala za mikoa na serikali za mitaa ambazo baada ya ugatuzi, mataifa mengine yameibua Kaunti kama sehemu ya maeneo ya utawala.

Lakini hatua hiyo inakuwa yenye kulinda maslahi binafsi na yanayohusu chama cha siasa. Kamwe hatua hizo hazigusi maslahi ya umma.

Ndio maana kwa watawala wa aina hiyo barani Afrika, hawajali umma unataka nini, umeamua nini na unaelekea wapi.

Inawezekana wananchi wakafanya uamuzi wa kuwachagua viongozi katika ngazi tofauti, wakiwaamini kwamba ‘wanatosha’ kuwaongoza au kuwawakilisha.

Licha ya ukweli huo, kikundi cha watu hasa walio na nguvu na mamlaka za utawala, kinaweza kuchukua hatua za udhibiti wa matakwa ya umma, kikageuza nia za raia walio wengi na kuzielekeza mahali panapowafaa.

Hali hiyo haiwezi kuleta umoja, haiwezi kuyafanya mataifa yakapata utulivu wa kisiasa, raia wake wakajikita katika kuwatambua na kuwashughulikia maadui wakiwamo wa kijamii.

Ndio maana mwenendo wa uchumi, maendeleo na ustawi wa mataifa mengi ya Afrika vimebaki vilipo, ama vimedidimia katika vipindi vya kutoka mwaka mmoja hadi mwingine.

Mataifa husika yameshindwa kutoka kwenye orodha ya nchi masikini, licha ya miongoni mwao kuwa na rasilimali nyingi za kuwezesha kukuza uwekezaji, uzalishaji wa bidhaa na huduma zinazohitajika kwa mataifa ya nje.

Wanasiasa hasa watawala wengi katika Afrika wanajali kuwapo kwao madarakani, hawaitazami jamii inayopaswa kujengwa katika misingi ya umoja utakaoyaweka kando maslahi ya kisiasa, kwamba kila raia anakuwa huru kuitumia ipasavyo haki ya kuchagua na kuchaguliwa.

Ikiwa mifumo, fikra na utashi wa wanasiasa katika Afrika utajikita huko, ni dhahiri kwamba kizazi kitarithishwa ushindani wenye tija, kwa kila anayechaguliwa kupimwa kwa misingi ya sera za kitaifa na ushirikiano wa kikanda na kimataifa.

Haiwezekani kwa taifa linaloendeleza mafarakano, kutanua wigo kati ya watawala na watawaliwa, likafikiria kwamba ipo siku litavuka hatua kuyaelekea maendeleo endelevu na ustawi bora wa watu wake.

Matumizi ya hoja zinazojenga chuki yanaendeleza chuki, ubaguzi unarithisha ubaguzi, mabavu yanazalisha wababe, hila ovu zinaeneza uovu na mengine mengi kama hayo.

Afrika inapaswa kutoka huko. Mataifa na tawala zao wasipokuwa na utashi thabiti katika kujenga umoja wa kitaifa, wakashindwa kuondokana na maslahi ya binafsi na yale ya kisiasa, jamii zake zikiwamo kizazi cha wanaosababisha kadhia hizo, hakitabaki salama kisiasa, kiuchumi na kijamii. Afrika itatafunwa kwa matendo hayo.

Mungu ibariki Afrika.
0754691540

Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo