Muswada wa Habari kuwasilishwa Bunge hili


Sharifa Marira, Dodoma

LICHA ya wadau wa habari kupinga kwa namna zote Muswada wa Habari kupelekwa bungeni, Serikali imedhamiria kuupeleka katika Bunge linaloanza leo ili kusomwa kwa mara ya pili, kuujadili na kuupitisha.

Spika wa Bunge, Job Ndugai, alisema hayo jana mjini hapa wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu ratiba ya shughuli za Bunge hilo ambalo linaanza leo hadi Novemba 11.

Ndugai alisema pamoja na Muswada huo, pia Serikali itawasilisha Muswada wa Marekebisho ya Sheria Mbalimbali, ambao pia utasomwa, kujadiliwa na kupitishwa.

Alisema pamoja na mambo mengine, Bunge litapokea Taarifa ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali(CAG), ya mwaka 2014/15 na majibu ya Serikali kuhusu ripoti hiyo.

Miongoni mwa majibu ya Serikali yanayosubiriwa kwa hamu ni utekelezaji wa maazimio ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), kuhusu ufisadi uliofanyika katika akaunti ya pamoja kati ya Tanesco na Kampuni ya kufua umeme ya IPTL (Escrow).

Alisema kamati mbili zinazohusu hesabu ambazo ni ya Hesabu za Serikali (PAC) na Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) zitawasilisha taarifa zao kutokana na vikao vya kamati hizo vilivyofanyika kwa wiki mbili na ripoti ya CAG ya mwaka 2014/15.

Mambo makubwa ambayo PAC itawasilisha ni suala la mkataba wa Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) kuhusu mradi wa ubia baina yake na Kampuni ya Azimio Housing Estates (AHEL), ambao umeonesha dalili za shirika kupoteza Sh bilioni 270.

Alisema wabunge watajadili na kushauri Serikali kuhusu makubaliano ya ushirikiano wa kiuchumi kati ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA) na Jumuiya ya Ulaya (AU) na kwamba Bunge linashauri Serikali ndiyo iwe yenye uamuzi wa mwisho.

Alisema Bunge hilo litakaa kama kamati kwa siku tatu mfululizo ili kupokea, kujadili na kutoa maoni yatakayosaidia kuweka vipaumbele kwenye bajeti ijayo ya Serikali, litapokea taarifa kutoa Kamati ya Sheria Ndogo.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo