Serikali yatangaza ukame, njaa


* Bei za vyakula nazo zapaa nchini

Waandishi Wetu, Dar na mikoani

OFISI ya Waziri Mkuu kupitia Idara ya Uratibu wa Maafa, imesema kuna dalili za nchi kukabiliwa na ukame utakaoandamana na kaya nyingi kukumbwa  na njaa na magonjwa ya mlipuko.

Kutokana na hali hiyo, imewataka wananchi kuchukua hadhari kwa kuotesha mazao ya muda mfupi na kutumia kwa uangalifu chakula walichonacho.

Akizungumza jana Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Idara hiyo, Brigedia Jenerali Mbaazi Msuya alisema hali hiyo inatokana na upungufu wa mvua na ukame unaoweza kuiathiri nchi.

Alisema hali hiyo inatokana na taarifa za Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA) kuonesha kwamba kutakuwa na ukame katika kipindi cha mwezi huu hadi Desemba.

Kwa mujibu wa Kaimu Mkurugenzi wa TMA, Dk Paschal Waniha kutakuwa na vipindi virefu vikavu ndani ya msimu wa mvua zinazoweza kusababisha unyevunyevu mdogo kwenye udongo na hivyo kuathiri ustawi wa mazao ya kilimo katika maeneo mengi nchini.

Kutokana na mtiririko huo mdogo wa maji, vina vya mito na mabwawa vinatarajiwa kupungua katika msimu wa vuli mwaka huu.

"Mlipuko wa magonjwa unaweza kujitokeza na uhaba wa maji salama na matumizi mabaya ya mifumo ya majitaka katika miji,” alisema.

Alisema uhaba wa malisho kwa wafugaji na wanyama unatarajiwa katika maeneo mengi ya nchi kutokana na kupungua kwa maji kwenye mabwawa na visima.

Uratibu   

Msuya alisema Idara ya Maafa inatoa hadhari kwa wizara, taasisi za Serikali, mamlaka za mikoa na wadau wengine wa usimamizi wa maafa, kuchukua hatua muhimu kukabiliana na tatizo hilo.

Alisema wakulima wanatakiwa kulima mazao ya muda mfupi na yanayostahimili ukame ikiwa ni pamoja na kuhifadhi.

"Pia nawasihi wananchi ili kukabiliana na kipindi hiki kuna haja ya kuchimba au kukamilisha na kukarabati mabwawa na malambo kwa ajili ya kuvuna maji ya mvua," alisema.

Brigedia Jenerali Msuya alisema maofisa ugani wote ambao wameajiriwa, sasa ni kipindi sahihi cha kufanya kazi rasmi ili kutoa ushauri kwa wakati kuhusu mazao ya kupanda.

Aliwataka wafugaji kuhifadhi chakula kwa ajili ya malisho ya mifugo na kuvuna mifugo, ikiwa katika hali nzuri kiafya, ili kupunguza idadi kubwa ya mifugo katika kipindi cha uhaba wa malisho ambapo inaweza ikafa kwa wingi na kupata hasara.

Pia alizitaka taasisi hizo kudhibiti usafirishaji holela wa mazao ya chakula kwenda nje ya nchi.

Usalama wa chakula

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Idara ya Usalama wa Chakula, Marystela Mtalo alisema idara yake itahakikisha inafanya kazi ya uratibu, ufuatiliaji, ukusanyaji na utoaji taarifa ya chakula nchini kwa wakati.

Alisema Bodi ya Nafaka inaelekeza nguvu kununua mazao ya wakulima kwa wingi ili kuongeza wigo wa biashara na soko la mazao ya wakulima, sambamba na kuyaongeza thamani.

Mtalo alisema mikoa na halmashauri zake zihamasishe na kufuatilia kwa karibu akiba ya chakula kwa wafanyabiashara ili kuwezesha kupata takwimu sahihi za kiasi cha chakula kilichopo nchini.

Alibainisha kuwa taasisi husika zihamasishe uwekezaji katika viwanda vya usindikaji mazao ili kuyaongeza thamani.

Uchunguzi uliofanywa na JAMBO LEO katika mikoa mbalimbali imeonekana kuwa hali ya upungufu wa chakula imeanza kujitokeza.

Limebaini kuwa wakulima katika mikoa ya kanda ya kati, Mashariki na Kaskazini hawakuvuna vyakula vya kutosha kutokana na ukame kuathiri mazao mengi, hasa mahindi na maharage.

JAMBO LEO lilitembelea baadhi ya maeneo ya Jiji la Dar es Salaam na kubaini kwamba bei ya mahindi imepanda kutoka Sh 650 kwa kilo mwezi uliopita hadi Sh 800 na Sh 1,000 mwezi huu.

Unga wa sembe umepanda kutoka Sh 24,000 kwa mfuko wa kilo 25 hadi kufikia Sh 27,000 na Sh  30,000. Unga wa sembe kwa bei ya rejareja nao umepanda kutoka Sh 1,000 hadi kati ya Sh 1,200 na  Sh 1,500.

Katika mkoa wa Ruvuma bei haijabadilika sana. Mahindi kwa kilo ni Sh  520 kwa wafanyabiashara wanaotoka nje, Sh 510 wafanyabiashara wa ndani na bei ya gunia la kilo 100 ni Sh 52,000.

Inasemekana bei hiyo inatokana na mahitaji ya chakula kwa baadhi ya nchi jirani na kuwa bei ya unga kwa kilo ni Sh 1,000 na mchele kilo ni Sh 2,200.

Katika mkoa wa Morogoro bei ya mchele inategemea  ubora wake ambapo bei inaanzia Sh 1,500 kwa kilo hadi Sh 1,000.

Mfanyabiashara Luth Kalikene wa Mbeya alisema kipindi cha mwezi wa mavuno walikuwa wakiuza kilo 20 sawa na debe moja kwa kati ya Sh 17,000 na Sh 18,000.

Kwa sasa alisema bei ya jumla ni kati ya Sh 25,000 hadi Sh 28,000 kutegemea na aina ya mchele huku bei ya reja reja ikipanda hadi Sh 32,000 kwa kilo 20.

Mkoani Kilimanjaro bei ya mahindi imepanda kutoka Sh 50,000 kwa gunia la kilo 100 hadi Sh 65,000.

Aidha, alisema kutokana na kupanda kwa bei ya zao hilo, unga wa mahindi umepanda kutoka Sh 1,000 hadi Sh 1,200 kwa kilo.

Mkoani Tanga mahindi gunia ni kati ya Sh 68,000 na Sh 70,000 tofauti na miezi miwili iliyopita ambapo liliuzwa chini ya Sh 60,000.

Kigoma mmiliki wa mashine za kusagisha nafaka,  Jiti Rubibi alisema mwanzoni mwa Septemba debe  la mahindi liliuzwa Sh 11,000 lakini sasa limepanda hadi Sh 13,000.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo