Magufuli aionya Bodi ya Mikopo

* Hataki kusikia mtoto wa tajiri akipata mkopo
* Ikilazimika atahakiki mwenyewe waliokopeshwa

Salha Mohamed

Rais Magufuli UDSM
RAIS John Magufuli ameionya Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (Heslb), kuwa akibidi ataitisha orodha ya wanafunzi wote waliopatiwa mikopo na kuhakiki mmoja baada ya mwingine yeye mwenyewe.

Akizungumza wakati katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), wakati akiweka jiwe la msingi katika ujenzi wa mabweni 20 yenye ghorofa nne ya chuo hicho, aliitaka Bodi hiyo, kuhakiki orodha ya wanafunzi wanaostahili kupewa mikopo ili kuepusha uwezekano wa wanafunzi wasiostahili hasa wa matajiri na mawaziri kupata mikopo hiyo.

“Sitaki siku nifike Bodi ya Mikopo nichukue orodha ya wanafunzi wote niangalie shule walizosoma na taarifa walizojaza, halafu nije nipewe majina ya watu ambao hawakustahili kupata mikopo.

“Wanafunzi 25,000 wa mwaka huu siwezi kushindwa kupitia kwa siku moja kwa kuangalia kurasa hadi kurasa kwani nitagawa (majina hayo) kwa saa 12 ambazo nitajifungia…tusifikie huko,” alionya na kuwataka wanafunzi kuwa wavumilivu katika kipindi wanachopitia sasa.

Alisema Serikali ilifuatilia Bodi hiyo na kubaini uwepo wa wanafunzi hewa pamoja na wanafunzi waliomaliza elimu zao lakini wakaomba mikopo upya, ili wapate fedha bila kuhudhuria darasani.

Alisisitiza kuwa Serikali haitatoa mkopo kwa wanafunzi wenye wazazi matajiri na badala yake wanaostahili ni watoto wa masikini, huku akiagiza Bodi hiyo kutumia sheria kudai walionufaika wa mikopo hiyo, kwani hadi sasa deni limefikia Sh trilioni 2.6.

“Lengo la Serikali ni kutoa elimu bora lakini haitatoa mikopo kwa wanafunzi wenye uwezo, mtoto wa Ndalichako (Profesa Joyce, Waziri wa Elimu, Sayansi na Mafunzo ya Ufundi) naye apate mkopo!

“Mtoto wa Katibu Mkuu Kiongozi Kijazi (Balozi John naye apate mkopo! Haiwezekani! Mkopo huu umelenga kwa ajili ya watoto masikini,”alisema Magufuli.

Alisema anafahamu na kusikia kuwa bodi ya mikopo kuna upendeleo wa kutoa mikopo kwani wapo wanaostahili kupata mikopo, lakini hawapati huku wasiostahili wakipata.

Alimtaka Profesa Ndalichako pamoja na Bodi hiyo kusimamia changamoto hizo na kuhakikisha Sh trilioni 2.6 zilizokopeshwa kwa wanafunzi zinarudishwa.

Katika hatua nyingine, Dk Magufuli amesema kumekuwepo na utitiri wa vyuo vikuu vinavyogombania wanafunzi, wakati baadhi ya  vyuo hivyo vikiwa na wanafunzi 20 bila mabweni wala mahabara.

“Natoa mwito kwa TCU, hebu mpitie vizuri…mnatoa vibali mno vya kuanzisha vyuo vikuu kila mahali wakati vyuo vilivyopo havijaja watu na vyuo vikuu vingine havina walimu,”alisema na kuongeza kuwa  si lazima kila mahali kuwe na chuo kwani  vingine vipo uchochoroni.

“Mimi nasema kwa uwazi siogopi, lazima tukae na tuchambue mwelekeo wa elimu…sisi serikali tumejipanga kutoa mikopo kwa watoto wa masikini.

“Wanahaki ya kuomba mikopo katika vyuo hivyo kwa sababu sisi ndiyo tumewapeleka huko, tumevuruga elimu tujirekebishe ili kuipa nafasi Serikali kwenda katika mwelekeo mzuri,”alisema.

Alisema haoni sababu ya kuwepo kwa mafunzo ya shahada ya udaktari katika Chuo Kikuu Dar es Salaam baada ya kuzinduliwa kwa Chuo cha Tiba cha Mloganzila  hivyo wanafunzi hao wapelekwe huko.

Aliongeza kuwa anafahamu mazingira wanayopitia wanafunzi hao kwa sasa kwani alisoma hapo, hivyo watimize wajibu wao.

“Waziri (Profesa Ndalichako) yale ambayo ni dosari, yamejitokeza yasijirudi tena, wanaostahili kupata mikopo wapate haraka na naninajua awamu ya kwanza zinahitajika zaidi ya Sh bilioni 157,” alisema.

Alisema awamu ya kwanza imetolewa Sh bilioni 80 na kuwataka wanafunzi hao kutumia fedha hizo kwa ajili ya kusoma.

Dk Magufuli alisema ni vema viongozi wa vyuo na wanafunzi waivumilie Serikali katika kupitia mabadiliko, ili kuweka utaratibu uliokuwa mzuri kwani anafahamu katika Bajeti ya Serikali ya 2016/2017 kulitenga Sh bilioni 340 zitakazotosheleza wanafunzi 90,000.

“Baada ya Serikali ya Awamu ya Tano kuingia madarakani ili kutimiza yale iliyoahidi tuliongeza fedha za mkopo hadi kufikia Sh bilioni 473 kutokana na makusanyo na kutoa mikopo kwa wanafunzi 124,358,”alisema.

Alisema mwaka huu zaidi ya Sh bilioni 480 zimetengwa ambapo wanafunzi wengi zaidi watapata mkopo huku akibainisha anafahamu wanafunzi waliokuwa wakiendelea pamoja na wanaojiunga sasa ni zaidi ya 25,000.

Magufuli alikiri kutokuwepo kwa uangalizi kwani vyuo vya elimu ya juu vinapaswa kuwa na tarehe moja ya kufungua, ili kuipa Bodi hiyo muda wa kutoa orodha ya wanafunzi wanaostahili kupewa mikopo.

“Palitakiwa kuwepo na Wizara ya Elimu, Wizara ya Fedha na Bodi ya Mikopo kwamba kuna wanafunzi watakaopata mkopo hawa, majina na kiasi cha fedha.

“Hapakuwa na sababu ya kufungua mwezi mzima kabla, wakati hawajui kama wanafunzi watapata mkopo au hawapati au asifanye udahili kwa sababu hajapata mkopo. Hii inaleta usumbufu kwa vijana,” alisema.

Awali akizungumza kabla ya kumkaribishwa Rais Magufuli, Profesa Ndalichako aliwataka wanafunzi kusoma na kucha kujiingiza kwenye siasa au kushabikia mambo yasiyokuwa na takwimu.

“Sasa hivi kumetokea upepo wa kusema vijana hawasomeshwi, mambo haya yametokea wapi? Kwa taarifa yenu hadi sasa hivi katika Sh bilioni 483 za Bajeti ya Serikali imeshatenga Sh bilioni 120,” alisema Profesa Ndalichako.

Alisema mchakato wa kutoa mikopo kwa wanafunzi unaendelea ambap hadi hadi sasa serikali imefanya malipo kwa wanafunzi 11,332 wa mwaka wa kwanza na Sh bilioni 40 zimeshatolewa kwa ajili ya ada vyuoni.

Alisema wanafunzi waliodahiliwa ni 58,000 huku akibainisha kuwa serikali haiwezi kutoa mkopo kwa mwanafunzi ambaye anauwezo.

“Wale waliokuwa kwenye utaratibu watapata fedha yao kama kawaida,tutafanya kazi kwa bidii bila kujali madongo ambayo tunapigwa ” alisema.

Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo