Abu Dhabi, Tanzania kukuza uhusiano


Mary Mtuka

Sheikh Mohamed bin Zayed Al Nahyan
MRITHI wa Mfalme wa Abu Dhabi na Kaimu Rais wa nchi hiyo, Sheikh Mohamed bin Zayed Al Nahyan, amesema nchi yake imedhamiria kuendeleza na kukuza zaidi uhusiano wake na Tanzania hasa katika utekelezaji miradi ya maendeleo.

Sheikh Mohamed alitoa ahadi hiyo jana kupitia kwa Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Maendeleo wa Abu Dhabi, Mohamed Al Suwaidi aliyekutana na kufanya mazungumzo na Rais John Magufuli Ikulu, Dar es Salaam.

Taarifa ya Ikulu iliyotolewa kwa vyombo vya habari Dar es Salaam, ilisema Mfuko wa Maendeleo wa Abu Dhabi unashirikiana na Tanzania katika utekelezaji wa miradi mbalimbali.

Katika mazungumzo yao, Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko huo, alionesha nia ya kushirikiana zaidi na Tanzania katika ujenzi wa miundombinu ya reli na barabara, usafiri wa anga na madini.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, pamoja na kumshukuru Mrithi huyo wa Mfalme Rais Magufuli aliialika nchi hiyo kupitia Mfuko wake na wadau wengine kuja kuwekeza nchini katika miradi ya maendeleo.

Alitaja baadhi ya maeneo ya kuwekeza kuwa ni ujenzi wa bandari, viwanda, kilimo, uvuvi, gesi na kushirikiana katika ujenzi wa Reli ya Kati ambayo itanufaisha nchi nyingine saba za Afrika Mashariki na Kati ambazo hazina bandari.

"Tanzania imeamua kujenga Reli ya Kati kwa kiwango cha kisasa na tayari katika bajeti yetu tumetenga Sh trilioni moja kwa ajili ya kuanza ujenzi, hivyo tunaukaribisha Mfuko wa Maendeleo wa Abu Dhabi kushirikiana nasi.

"Wapo wengi waliojitokeza kushirikiana nasi lakini na nyie tunawakaribisha, mnaweza kuchukua sehemu ya reli na mkajenga," alisema Rais Magufuli.

Aidha, Dk Magufuli aliutaka Mfuko huo kufupisha muda unaotumika kwenye mchakato wa kuanza utekelezaji wa miradi ili kuharakisha matokeo yake na manufaa kwa wananchi.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo