Nusu ya wanafunzi wakosa mikopo


*Wanufaika wa zamani 93,295 wachekechwa upya

Suleiman Msuya

Mwanafunzi akilia kwa kukosa mkopo
NUSU ya wanafunzi wa mwaka wa kwanza walioomba mikopo ya elimu ya juu wamekosa, huku mamlaka zikiendelea kuwachunguza wanafunzi wengine 93,295 waliokuwa wakinufaika na mikopo hiyo kuona kama kweli walistahili kupata au la.

Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB), Abdul-Razaq Badru alisema jana jijijini Dar es Salaam kuwa wanafunzi 25,717 wa mwaka wa kwanza pekee ndiyo watakaopata mikopo kwa mwaka wa masomo 2016/17 kati ya wanafunzi 58,000 ambao majina yao yaliwasilishwa kwake na Tume ya Vyuo Vikuu Nchini (TCU).

Alisema mbali na hilo, bodi hiyo pia inahakiki majina ya wanafunzi 93, 295 waliokuwa wananufaika na mikopo hiyo ili kujiridhisha kama kweli walistahili kulingana na vipaumbele vya serikali na watakaobainika kukosa sifa wataondolewe kwenye mfumo na kutakiwa kurudisha fedha.

Badru alisema kuwa bodi hiyo inatarajia kuhakiki taarifa za wanafunzi wote wanaondelea na masomo ili kubaini uhitaji wao wa sasa na kwamba watakaokosa sifa stahili wataondolewa kwenye mfumo wa kukopeshwa.

“Watakaondolewa katika mchakato wa kupata mikopo, watalazimika kurejesha kiasi walichokopeshwa kuanzia mwezi huu,” alisema Badru.

Alisema katika kutoa mikopo wamekuwa wakitumia vigezo mbalimbali, vigezo hivyo vitatumika ili wanufaika wanaostahili waweze kupatiwa mikopo na ambao hawastahili waendelee kujilipia.

Alipoulizwa haoni kama uamuzi huo utaibua mgongano kwa kuwa wanafunzi hao walianza kupewa mikopo mwaka jana kwa kuzingatia vigezo ambavyo walikidhi, Badru alisema wanachoangalia kwa sasa ni kujiridhisha na taarifa ili kuweka mambo sawa.

“Sisi wenyewe watumishi tunahakikiwa, hivyo lengo la kuwahakiki wanufaika ni kutaka kuhakikisha kuwa wanaostahili wanapata mikopo na wale ambao wanajiweza wajilipie kama wanasoma masomo yasiyo na vipaumbele,” alisema.

Badru alisema bodi ya mikopo baada ya kupitia taarifa za waombaji ilibaini kuwa wapo wanafunzi ambao historia yao inaonesha walisoma shule za gharama na wanapata mikopo, hivyo ni wakati wa kuachana na kundi hilo kama litakuwa halina vigezo husika.

Aidha, alisema uhakiki huo utaangalia vipaumbele vya taifa, familia maskini, yatima, waliosomeshwa na taasisi na walemavu, hivyo wahusika wakiwa si katika makundi hayo wanaweza kufutiwa mikopo.

Mkurugenzi huyo alisema uhakiki huo unaweza kusaidia wale ambao walikuwa wanapata mkopo kidogo na wanakidhi vigezo kuongezewa.

Kuhusu wanafunzi watakaonufaika na mikopo alisema bajeti ya Serikali kwa mwaka 2016/17 ni Sh. Bilioni 483 itahusu wanafunzi 25,717 wa mwaka wa kwanza na wanaondelea ni 93, 295 ambao watakuwa katika uhakiki.

Alisema hadi sasa wanafunzi wa mwaka kwanza ambao wamepatiwa mikopo ni 20, 391 na orodha za majina hayo zimetumwa katika vyuo mbalimbali walivyopangiwa na TCU.

Badru alibainisha mgawanyo wa mikopo hiyo kuwa ni yatima 4,321, walemavu 118, waliofadhiliwa na taasisi 295, wanaosoma kozi za vipaumbele 6,159 na wanaotoka familia duni 9,498.

Alisema nafasi zilizobakia ni zaidi 4,500 ambazo zitajazwa na wanafunzi waliokata rufaa na wanaodahiliwa upya na TCU na kuwa jumla ya wanufaika wapya watakuwa 25,717 kwa mwaka huu wa fedha.

Aidha, alisema idadi ya wanufaika inaweza kuongezeka au kupungua mwakani hali ambayo itachangiwa na uhitaji na vigezo ambavyo vitatumika.

Badru alisema ofisi yao itapokea rufaa za waombaji ambao hawakuridhika na matoke ya upangaji wa awamu ya kwanza na kuwa mchakato huo utaanza Novemba 2 mwaka huu na kumalizika baada ya siku 90.

Kwa upande mwingine mkurugenzi huyo alitaja waombaji 27, 053 ambao wamekosa mikopo kuwa ni 6,581 hawakuomba mikopo pamoja na kuwa na sifa, 8,781 waliofuzu kama wahitimu binafsi.

“9, 940 wahitimu waliofuzu kwa vigezo wianishi, 1,416 wasiokamilisha maombi, 245 walimaliza kidato cha tano miaka mitatu iliyopita na 90 wenye miaka zaidi ya 30,” aliongezea

Halikadhalika alisema kuhusu taarifa za wanufaika walizotuma wakati wa kuomba na kupangiwa mikopo uhakiki utafanyika kwa njia ya dodoso ambapo kila mnufaika atalazimika kujaza dodoso hilo kwa njia ya mtandao kupitia akaunti yake.

Kwa upande wake Rais wa Wanafunzi wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM), Kilonzo Mringo alisema bodi ya mikopo inapaswa kutafakari upya uamuzi wake wa kukutaka kufutia baadhi ya wanafunzi mikopo.

Mringo alisema bodi hiyo inapaswa kuendelea na utaratibu wa mikopo kwa wanafunzi wanaondelea na kama yapo mabadiliko yahusu wanafunzi wapya.

Alisema wapo wanafunzi wanalipa ada inayobakia kupitia fedha za matumizi ambazo wanapewa na bodi hivyo uamuzi huo utagharimu wanafunzi wengi.

“Mimi nashauri bodi kama inahitaji kuhakiki ihakiki kwa msingi wa kuangalia au kujiridhisha na wanufaika na si kuwaondolea wanufaika mikopo hii ni tatizo kwa sababu mikopo hiyo inasaidia sana,” alisema.

Dk. Chris Mauki wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), alisema iwapo mwanafunzi analipewa mkopo kulingana na vigezo ambavyo vilihitajika wakati huo kumuondolea mkopo itakuwa si sahihi.

Alisema kama bodi itabaini kuwa kuna mapungufu au vigezo baadhi kutofuatwa uamuzi wa kumuondolea mkopo unapaswa kuchukuliwa bi al kuhurumia mtu.

“Wapo wanafunzi ambao wanadanganya taarifa zao wakati wakuomba hivyo wakibainika ni sahihi bodi kufanya hivyo ila si sahihi kwa dhana kuwa hasomi masomo ya kipaumbele je wakati anaomba kulikuwa na mazingira hayo,” alisema.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo