CCM sasa yataka Zitto apekuliwe


Waandishi Wetu

Zitto Kabwe
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimeitaka Serikali kuhakiki akaunti na mali za Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT) na wenzake waliokuwa katika kamati za fedha za Bunge, ili kubaini kama zinalingana na kipato walichokuwa wakipata.

Msemaji wa chama hicho, Christopher Ole Sendeka, amesema hayo jana alipozungumza na waandishi wa habari, akimuhusisha Kiongozi huyo Mkuu wa ACT na tuhuma za ufisadi wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), alipokuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC).

”Nilikuwa najiuliza hivi chuki ya Zitto kwa Serikali ya Awamu ya Tano, inayopambana na mafisadi imetoka wapi wakati yeye alikuwa anasimamia mashirika hayo.

“Miongoni mwa taasisi hizo alizokuwa akisimamia na baadhi ya marafiki zake ndiyo hao walionunua hekari moja kwa Sh milioni 800, wakati ilikuwa ikiuzwa kwa Sh milioni 25 na walikuwa wamejificha kwa maslahi binafsi,” alisema katika ofisi ndogo za Makao Makuu, Lumumba Dar es Salaam.

NSSF ndiyo iliyonunua hekari 20,000 Kigamboni jijini Dar es Salaam kwa Sh milioni 800 kwa kila hekari, badala ya Sh milioni 25 na kujikuta katika hatari ya kupoteza Sh bilioni 270, katika mradi wa ujenzi wa mji wa kisasa wa Dege Eco Village.

Kutokana na tuhuma hizo za NSSF zilizoibuka upya katika kamati ya PAC wiki hii, Sendeka alisema ni vema Serikali ikague  kuona kama akaunti za viongozi wa zamani wa kamati hizo, maisha yao na mali walizonazo, zinafanana na mapato halali waliyokuwa wakilipwa.

Alisema alikuwa anaangalia msukumo wa ghafla na mapenzi ya akina Zitto waliyokuwa wanayapata kwa nchi, kumbe ilikuwa ni kichaka cha kuficha baadhi ya maswahiba zao wasichukuliwe hatua.

Aliwahakikishia wananchi kuwa Serikali ya Rais Magufuli haina nia ya kurudi nyuma katika jambo lolote na kuwa itasonga mbele huku akiamini kuwa Serikali iliyochaguliwa na watu haiwezi kufa.

“Tunahakika Serikali ya Magufuli iliyopata ridhaa ya kutumikia watu, haitafutika kwa kelele za mlango wa baadhi ya makuwadi na watu waliolipwa kuchafua taswira ya Tanzania,” alisema.

Aliongeza kuwa Serikali hiyo itaendelea kushughulikia wakwepa   kodi pamoja na kuchunguza mambo aliyoanzisha Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alipokuwa bandarini.

*Kauli ya Zitto

Akizungumza na waandishi wa gazeti hili, Zitto alisema hana muda wa kujibu alichoita kuwa ni porojo na viroja vya Sendeka.

Alifafanua kuwa CCM ni chama dola na kuna taasisi nyingi za uchunguzi za Serikali, ikiwemo Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru) na Mkurugenzi wa Mashitaka ya Jinai (DPP) na kushangaa kwa nini vyombo hivyo havisemi, aseme Sendeka?
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo