Lissu: Watawala wanajimaliza wenyewe


Mwandishi Wetu

Tundu Lissu
MBUNGE wa Singida Mashariki na Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu, amesema vitendo vya uminyaji demokrasia na ubabe vinavyofanywa na watawala vinawamaliza.

Lissu alisema hayo kwenye waraka wake aliouandika baada ya kudai kupokea ujumbe tofauti 297,576 kutoka kwa wananchi   wakihoji sababu za vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) na Chadema kutochukua hatua kwa wanayotendewa.

Alitaka wananchi na wafuasi wa vyama vyao kuvuta subira kwa kile anachoamini kuwa hakuna lisilo na mwisho katika dunia.

“Mnakumbuka Rais wa zamani wa Ivory Coast, Laurent Gbagbo alivyoshindwa uchaguzi akalazimisha tume ya uchaguzi imtangaze ameshinda, na tume kwa sababu haikuwa huru, ikamtangaza mshindi badala ya Alassane Ouattara na sasa ameshitakiwa kwenye Mahakama ya ICC, kwa hiyo haya ni mambo ya muda tu,” alisema.

Alitolea mfano wa pili wa Samwel Doe wa Liberia ambaye alipinduliwa na rafiki yake aliyekuwa na jeshi dogo lakini wananchi walimwunga mkono kutokana na kupinga udhalimu uliotendewa na watu.

Lissu alisema wapinzani hawapendi kuingia kwenye vurugu za kuhatarisha amani ya nchi ingawa wanabambikiziwa kesi za uchochezi kila kukicha.

Alisema jambo la kusikitisha ni kusikia kesi hizo wanazobambikiziwa kuwa ni maagizo kutoka juu, hivyo wao wanatimiza.

“Ila niwaambie neno moja tu kutokana na utafiti huu  wanajimaliza wenyewe, huku wapiga vigelegele wao wakiwapoteza,” alisema.

Alisema si watu wote walio kwenye mfumo wanaofurahia wanayofanyiwa hivyo wanawapa taarifa za mambo wanayotaka kuwafanyia.

Mbunge huyo aliwataka wafuasi wao kutambua kuwa mambo hayo ni mazito na wasikimbilie hasira, kwani ni hasara.

“Waonevu wengi huwa na chuki na visasi nyoyoni na vitu wanavyofanya ni kwa malengo yao maalumu,” alisema.

Mwanasheria huyo alisema watawala wanaweza kuweka kikwazo fulani au kitu fulani vurugu itokee ili wapate sababu au kisingizio cha kumpata mtu fulani na kulinda maslahi yao.

Lissu alisema watawala wanapanga kukamata mtu na kumtia kizuizini ili lengo litimie kama ushindi wa uchaguzi, au vinginevyo, na pia kuvipunguzia nguvu vyama au kuviua,” alisema.

Alisema hata vitendo vya kukwamisha miradi ya maendeleo katika maeneo ambayo yanaongozwa na wapinzani ni moja ya mikakati ya watawala kutengeneza migogoro baina yao ila wao wako makini.

“Napenda niwasihi makamanda wote na wapenzi wa UKAWA tuwe na busara kwani Afrika tuko kwenye hali mbaya sana, na tufahamu kuwe watawala wanajimaliza, ni suala la muda tu,” aliongeza.

Alisema kila kona na kila idara ni vilio na kwa mujibu wa utafiti aliofanya ni wazi kuwa wanajimaliza kwa umma.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo