Bunge: PSPF inachungulia kaburi


Sharifa Marira, Dodoma

MFUKO wa Pensheni wa PSPF uko kwenye hali mbaya kifedha kutokana na kupata hasara inayofikia Sh trilioni 11.15 hivyo Serikali imetakiwa kuchukua hatua za haraka za kuuokoa kwa kulipa madeni yake.

Agizo hilo lilitolewa juzi na Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) wakati inapitia hesabu za shirika hilo za mwaka 2014/15.

Ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka huo, zinaonesha kuwa una hasara ya Sh tilioni 11.15, kutokana na Serikali kuchelewa kulipa madeni ya mafao ya wanachama waliokuwapo kabla ya kuanzishwa kwa Mfuko huo Julai, 1999.

Kwa mujibu wa taarifa ya CAG shirika hilo lisipookolewa litaelekea kufa kutokana na ukweli kuwa kwa mwaka huo wa fedha unaoishia Juni 2015, lilipata hasara ya Sh trilioni 11 badala ya faida.

Wakati PAC ikipitia hesabu hizo za CAG, ilibaini kuwa pamoja na kupokea michango ya wanachama wake inayofikia Sh bilioni 661 kwa mwaka, inalazimika kulipa mafao yanayofikia Sh bilioni 663 na hivyo upungufu wa ulipaji deni hilo kwa Sh bilioni mbili.

Mbunge wa Vwawa, Japhet Hasunga (CCM) alisema kiasi ambacho Mfuko huo unakusanya na matumizi yake hasa kwa kulipa mafao hakitoshelezi, kwani kwenye mafao pekee, kuna upungufu wa Sh bilioni mbili.

‘’Mwaka 2010 walikuwa na nakisi ya Sh trilioni 6.2 na sasa mwaka 2014 imeonekana nakisi ya Sh trilioni 11.6, hatua za haraka zisipochukuliwa, Mfuko huu unaelekea kufa wa kuuokoa ni Serikali ambayo inadaiwa,” alisisitiza.

Alisema mwaka 1999 wakati Mfuko unaanzishwa, Serikali iliupa wafanyakazi takriban 700 ambao haikuwachangia chochote kwenye Mfuko na kukubaliana na PSPF kuwa italipa Sh bilioni 710.

Alisema hata hivyo, Serikali haikulipa deni hilo na baadaye iliingia mkataba na Mfuko kulipa Sh bilioni 71 kila mwaka, jambo ambalo pia halikutekelezwa zaidi ya kulipwa fedha kidogo na kusababisha deni hilo kukua na kufikia Sh trilioni 2.6.

Mbunge wa Sikonge, Joseph Kakunda, alisema kwa mujibu wa ripoti ya CAG na deni hilo la mafao ya wastaafu wa mwaka 1999, pia Mfuko una madai ya mikopo kutoka taasisi za Serikali ya Sh bilioni 499.7.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dorothy Mwanyika alisema Serikali inalitambua deni la PSPF, na itaanza kulilipa kupitia njia ya hati fungani kuanzia Februari mwakani.

Mwanyika alisema kuhusu deni la wafanyakazi wa mwaka 1999, Serikali itaanza na utaratibu wa kuhakiki deni hilo ndipo ianze kulilipa kwa kutumia hati fungani za miaka mitatu hadi 20.

Alisema malipo hayo yatajumuisha madeni ambayo Mfuko umechangia katika miradi mikubwa ukiwamo ujenzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM).
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo