CUF, Chadema wapinga umeya wa CCM kortini

Grace Gurisha

Wakili John Malya
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam inajipanga kutoa tarehe rasmi ya kuanza kusikiliza kesi ya kupinga matokeo ya umeya wa Kinondoni, ambayo yalimpa ushindi Benjamin Sitta, iliyofunguliwa na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).

Hatua hiyo inakuja baada ya kesi hiyo namba 3 ya mwaka huu kupangiwa hakimu ambaye ni Hakimu Mkazi Mkuu, Respicius Mwijage wa Mahakama hiyo.

Wakili wa Chadema, John Malya, alisema jana kuwa walifungua kesi hiyo baada ya juzi kushindwa kufanya hivyo kwa sababu muda wa kazi ulikuwa umepita, kwa hiyo wanasubiri Mahakama ipange tarehe.

Mbali na Sitta ambaye alipata kura zote 18 walalamikiwa wengine katika kesi hiyo ni Naibu Meya George Manyama (CCM), Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kinondoni, Aron Kagurumjuli na Ofisa Tawala wa Manispaa hiyo.

Alisema walifikia uamuzi wa kwenda mahakamani kutokana na mchezo mchafu waliochezewa na CCM katika uchaguzi huo uliofanyika Oktoba 23 ukiambatana na kukiukwa kwa sheria na taratibu ambazo zilitakiwa kufuatwa.

Malya alisema wanaiomba Mahakama itengue umeya wa Sitta, kwa sababu CCM walikaaa wenyewe na kujichagua kutokana na mambo yao ambayo waliyapanga katika kikao hicho, hali ambayo ilisababisha wao wagomee kikao hicho.

"Tunaiomba Mahakama iamuru uchaguzi wa Meya ufanyike mara moja kwa kufuata kanuni, kisije kikatokea kama kilichotokea awali kwa CCM kupanga matokeo," alisema Malya.

Pia alisema katika hati yao wanaiomba Mahakama iwaamuru Kagurumjuli na wasimamizi wote wa uchaguzi wafuate taratibu za kisheria.

Aliongeza kuwa wanaiomba pia Mahakama iwaamuru wadaiwa walipe gharama za kesi huku akisema pia walalamikaji katika kesi hiyo ni Diwani wa Kata ya Kinondoni, Mustafa Muro ambaye pia alikuwa mgombea na aliyekuwa Naibu Meya Jumanne Mbunju.

Katibu wa Chadema Dar es Salaam, Henry Kileo alisema walikimbilia mahakamani kwa sababu haki yao iliporwa wazi wazi.

Alisema kilichosababisha uchaguzi wa Ubungo kuahirishwa ni  kukiukwa taratibu hivyo Mkurugenzi wa Ubungo na Ofisa Tawala wa Ubungo waliahirisha uchaguzi huo baada ya kubaini kuna taratibu zilikiukwa kama zilivyokiukwa Kinondoni.

Kileo alisema Kinondoni walitumia ubabe na kushindwa hata kusikiliza malalamiko ya madiwani, ambao ndio waliwasilisha malalamiko yao Ubungo wakaahirisha uchaguzi.

Pia alisema Mkurugenzi hana mamlaka ya kuandaa kikao, kilichofanyika juzi kuchagua Mwenyekiti na si Meya kwa sababu akidi haikutimia.

"Madiwani wetu walikataliwa kuingia Manispaa jambo ambalo si haki kabisa, kwa hiyo nawaambia Ukawa wote hatumtambui Sitta kama Meya, Kinondoni hivi sasa haina Meya. Kama tulivyoanza mitaani, tukaja mahakamani, tutarudi tena mitaani ili tuendelee kuitafuta haki yetu," alisema Kileo.

Mbunju alisema kilichofanyika juzi ni mkusanyiko wa watu walioamua mambo yao kwa kuchaguana, kwa hiyo uchaguzi huo ni haramu.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo