Tanesco yaichongea Serikali kwa wabunge


Sharifa Marira, Dodoma

Felchesmi Mramba
SHIRIKA la Umeme Tanzania (Tanesco), limeichongea Serikali mbele ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) likieleza kuidai Sh bilioni 125 kutokana na taasisi zake kubwa kutumia umeme bila kulipa.

Akizungumza mbele ya Kamati hiyo jana mjini hapa, Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Felchesmi Mramba, alilitaja Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO) kuwa ndilo mdaiwa sugu wa Sh bilioni 85 huku taasisi zingine zikidaiwa Sh bilioni 40.

Mramba alisema hayo wakati akijibu hoja za wajumbe wa PAC kuhusu ripoti ya ukaguzi ya CAG iliyoishia Juni mwaka jana ya hesabu za shirika hilo.

Alisema shirika hilo limeanza kufanya mikutano kadhaa na ZECO kwa ajili ya mikakati itakayofanikisha kulipwa deni hilo la tangu mwaka 2013.

Katika mikutano hiyo walibaini kuwa ZECO inashindwa kulipa kwa sababu inatoza gharama ndogo kwa wateja wa umeme Zanzibar tofauti na gharama za ununuaji umeme kutoka Tanesco.

Mramba alisema kwa taarifa za hivi karibuni ambazo shirika hilo lilizipata kutoka ZECO ni kwamba limewasilisha deni hilo kwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ili kusaidiwa kulipa.

Msajili wa Hazina, Lawrence Mafuru alisema tayari amewasilisha ripoti ya madeni hayo ngazi za juu za uamuzi kwa ajili ya kufanyiwa kazi,Tanesco imefanya jitihada kubwa sana katika kuhakikisha inalipwa madeni haya.

Alisema katika kipindi cha wiki mbili zilizopita, waliwasilisha suala hilo ngazi za juu za uamuzi na kueleza changamoto zinazolikabili shirika hilo za kutokulipwa madeni yake hasa na taasisi kubwa za Serikali.

Mafuru alieleza kuwa maelekezo ya ngazi hizo za juu ni kwamba kuanzia sasa taasisi yoyote isiyotenga bajeti yake kwa ajili ya umeme, isipolipa ichukuliwe hatua.

Mwenyekiti wa PAC, Naghenjwa Kaboyoka aliiagiza Serikali kuhakikisha inalipa madeni hayo ya Tanesco ndani ya miezi sita.

Mbunge wa Morogoro Mashariki, Omary Mgumba (CCM) alilitaka shirika hilo, pamoja na kufuatilia madeni hayo, liweke mikakati ya kuhakikisha linaondokana na tatizo la mlundikano wa madeni, hali inayosababisha liendelee kujiendesha kwa hasara.

Mramba alisema kwa sasa limeanza kuondoa mita zote za kawaida na kuweka za mfumo wa Lipa Kadri Unavyotumia (LUKU).
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo