Majaliwa apongeza makanisa kujenga Dodoma


Mwandishi Wetu

Kassim Majaliwa
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa ameeleza kufurahishwa na uamuzi wa Kanisa Katoliki na Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) kutafuta viwanja Dodoma ili kujenga ofisi za makao yao makuu na makazi ya viongozi wao wakuu.

Alitoa kauli hiyo jana alipozungumza na Askofu wa Jimbo Katoliki la Dodoma, Mhashamu Beatus Kinyaiya na Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kikristo ya Huduma za Kijamii (CSSC), Peter Maduki ofisini kwake Dodoma.

“Sina shaka juu ya maombi yenu ya kupewa viwanja kujenga makao makuu na makazi ya viongozi wakuu. Sasa hivi mpango wa Dodoma kama makao makuu ya nchi inapitiwa upya, ili izingatie mahitaji ya msingi kwa sababu zamani ilikuwa haijapangwa kwa mazingira ya sasa ya ujio wa Serikali,” alisema Waziri Mkuu.

Alisema wiki tatu zilizopita, alimwagiza Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA) atafute kampuni zenye uwezo wa kupima viwanja haraka.

“Hii itatusaidia kutambua tuna eneo kiasi gani na mahitaji halisi ni yapi na nani akija apewe eneo lipi kulingana na mahitaji yake,” aliongeza.

Awali Askofu Kinyaiya alimweleza Waziri Mkuu kwamba wanahitaji eneo la kujenga ofisi za makao makuu na makazi kwa ajili ya Kanisa na makanisa yaliyo chini ya CCT ambayo kwa pamoja yanaunda Tume ya Kikristo ya Huduma za Kijamii (CSSC).

Alisema wanahitaji eneo kwa ajili ya ujenzi wa ofisi, pia makazi ya Balozi wa Baba Mtakatifu nchini.

Alisema walipowasilisha maombi yao CDA, waliahidiwa kupewa eneo la makazi tu, lakini bado wanahitaji eneo la ofisi.

Pia alitumia fursa hiyo kumshukuru Waziri Mkuu kwa alivyoiwakilisha Serikali kwenye maziko ya Mhashamu Askofu mstaafu Mathias Isuja wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dodoma ambaye alifariki dunia Aprili 13 na kuzikwa Aprili 20.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu alishukuru makanisa kwa huduma za kijamii zitolewazo katika sekta za elimu, afya na kilimo kama alivyoshuhudia katika baadhi ya maeneo nchini.

Pia aliwakubalia maombi ya kikao cha pamoja baina ya watendaji wa Serikali na makanisa ambacho kitajadili namna ya kuimarisha ubia katika utoaji wa huduma za kijamii hususan kwenye afya na elimu.

“Kikao hiki kitafanya mapitio ya huduma zinazotolewa baina ya Serikali na Makanisa, lakini pia kitatusaidia kupata mrejesho wa mambo yanayofanyika kwenye hospitali na shule mnazomiliki katika maeneo mbalimbali nchini,” aliongeza.

Alitaka waharakishe kuleta mapendekezo yao ili kikao hicho kifanyike kabla ya Desemba, mwaka huu, kwani kitaisaidia Serikali kupata mrejesho wa kuboresha baadhi ya maeneo katika mwaka mpya wa kielimu unaoanza Januari kila mwaka.

Katika mkutano huo, Maduki alisema katika sekta ya afya hadi Juni, makanisa yalikuwa yanamiliki na kuendesha hospitali 102, vituo vya afya 102 na zahanati 696.

“Kati ya hospitali 102, mbili ni za rufaa za kanda na 38 ni za hospitali teule za halmashauri za wilaya na hospitali zingine 62 zinatoa huduma halmashauri mbalimbali,” alisema.

Alisema karibu asilimia 38 ya hospitali nchini zinamilikiwa na makanisa na nyingi ziko maeneo ya vijijini. Pia alisema kuna chuo kikuu kimoja, vyuo vikuu vishiriki vitatu, na vyuo vya mafunzo ya kati 62 ambavyo vinatoa kozi za uuguzi, maabara na ufamasia.

Kuhusu sekta ya elimu, Maduki alisema makanisa yanatoa elimu kuanzia ya awali hadi chuo kikuu na kwamba hadi kufikia Juni, 2016, makanisa yalikuwa na shule za msingi 161, za sekondari 369, na vyuo vya ufundi stadi 126.

“Pia tuna vyuo vya ualimu 14, vyuo vikuu tisa, vyuo vikuu vishiriki 17 na vituo vya vyuo vikuu saba,” alisema.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo