Abiria walalamikia mabasi yaendayo haraka


Abraham Ntambara

BAADHI ya wakazi wa Jiji la Dar es Salaam wamelalamikia huduma za Kampuni ya Mabasi Yaendayo Haraka (UDART), wakisema haziridhishi na zimekuwa zikitolewa kwa kusuasua.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na gazeti la JAMBO LEO jana, wakazi hao walisema huduma si ya kuridhisha kutokana na kukaa vituoni muda mrefu wakisubiri usafiri huo.

Saumu Shaibu alisema hali hiyo hujitokeza mara nyingi asubuhi na jioni watu wakienda kazini na wanafunzi shuleni na jioni wanaporudi nyumbani.

“Jioni na asubuhi ndiyo kwa kiasi kikubwa tatizo hilo hujitokeza kwa maana hiyo tunakuwa wengi kwenye vituo na tunakaa kwa muda mrefu huku magari yakionekana kuwa machache,” alisema Saumu.

Moses James alisema kwa jinsi wanavyokumbwa na adha hiyo inaonekana kana kwamba magari yamepungua barabarani, kutoa huduma hiyo hali inayosababisha kuwa machache na hivyo kutoa huduma isiyokidhi mahitaji ya wasafiri.

“Magari yanaonekana kama yamepungua, ni machache ikilinganishwa nasi watumiaji wa huduma hii, wakazi wa Dar es Salaam ambao ndio watumiaji kwa kiasi kikubwa wa huduma,” alisema James.

Aidha, aliongeza kuwa kutokana na hali hiyo, wamekuwa wakijikuta wanavuruga ratiba zao kwa kuwa wanachelewa  shughuli zao wakati walikuwa wanaamini usafiri huu kwa kiasi kikubwa ungewaondolea adha ya upotevu wa muda na kufanya shughuli zao za kiuchumi.

Halfan Rashid aliongeza kuwa bado tatizo la chenji pia limeendelea kuwa kero kwa kuwa sehemu za nauli ya Sh 650 wamekuwa wakilipa Sh 700 huku wanapokatisha tiketi za mabasi hayo wakisema hawana Sh 50 za kuwarudishia.

“Kwa kweli hili ni tatizo na tunalilalamikia kwa muda mrefu wao hawaoni wajibu wa kutafuta hizi chenji, lakini sisi ndio wanatwambia tuje nazo na kama huna kamili hawarudishi chenji, mbona wao tukiwa na pungufu hawaturuhusu?” Alihoji Rashid.

Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili ulibaini kwamba kampuni hii inajiendesha kwa hasara na ndiyo maana huduma zake zinakuwa za kusuasua.

Ofisa Habari wa UDARTDeus Bugaywa alipoulizwa kuhusu madai ya kampuni kujiendesha kwa hasara, alisema hawezi kuzungumzia hilo kwa kuwa halijatolewa na uongozi wa Kampuni na kubainisha kwamba kila mtu anaweza kuzungumza analojua.

“Nani kasema, taarifa hizo umezitoa wapi? Hebu jaribu kufanya tathmini tena halafu uulize. Mimi siwezi kuzungumzia hilo kwa kuwa halijatolewa na uongozi na kila mtu anaweza kuzungumza analojua yeye,” alisema Buganywa.

Aidha, kuhusu malalamiko ya abiria kuchelewa kwenye vituo na mabasi kupungua, alisema anavyofahamu ni kwamba kila mtu anajua idadi ya mabasi yaliyoko barabarani kutoa huduma.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo