Wenye viwanda watakiwa kushiriki maonesho


Celina Mathew

Charles Mwijage
SERIKALI imetaka Watanzania wanaomiliki viwanda vidogo, vya kati na vikubwa, washiriki maonesho ya viwanda nchini yanayotarajiwa kuanza Desemba 7 hadi 11 kwenye viwanja vya maonesho vya Mwalimu Julius Nyerere, Dar es Salaam.

Maonesho hayo yenye kaulimbiu ya: ‘Tanzania Sasa Tunajenga viwanda’, lengo lake ni  kuwaaminisha wananchi juu ya falsafa na  ujenzi wa uchumi wa viwanda na kuwahamasisha kuthubutu kujenga viwanda kwa kuwakutanisha walioanza siku nyingi na wapya.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage alisema lengo la maonesho hayo ni kuhakikisha Tanzania inakuwa nchi ya viwanda ifikapo mwaka 2025, pamoja na kujenga jukwaa la wadau wa sekta ya viwanda kupata fursa ya kujadiliana, kubadilishana uzoefu na kutangaza fursa zilizopo.

Alisema pia yatatoa fursa za kutoa taswira ya juhudi za ujenzi wa viwanda kwa kipindi cha mwaka mmoja uliopita, kutangaza bidhaa na huduma zinazotolewa nchini ili kutoa hamasa kwa Watanzania kutumia bidhaa na huduma za viwanda vya ndani.

Aidha, alisema yataunganisha wenye viwanda na wazalishaji wa malighafi na huduma zingine za viwandani, kutoa semina na mijadala ya kitaalamu ikihusu maendeleo ya viwanda nchini, kutangaza fursa za masoko ya ndani na nje na kuwezesha watafiti na wabunifu kujadiliana na wenye viwanda juu ya kuboresha teknolojia za uzalishaji na Tehama.

Nyingine ni kuwezesha vijana na wanafunzi kuchangamkia fursa za ajira na masomo ya masuala ya viwanda ikiwamo kuwajengea tamaa ya kuanzisha  viwanda, kutoa fursa kwa wananchi kutambua viwanda vilivyopo na kuwatia hamasa ili kuwekeza katika viwanda na mamlaka husika zinazotumia maonesho hayo kutangaza fursa za uwekezaji katika mikoa yote ya Tanzania yakiwamo maeneo ya kujenga viwanda.

 “Kama mnavyojua mpango wa pili wa miaka mitano unatamka wazi kuwa sekta binafsi ndiyo mhimili wa ujenzi wa uchumi wa viwanda, hivyo maonesho haya mhusika mkuu ni sekta binafsi na Serikali ni wawezeshaji,”alisema.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo