Shahidi adai hakupata wakala wa CCM kwenye majumuisho


Adda Ouko, Musoma

Tundu Lissu
ALIYEKUWA Msimamizi wa Uchaguzi jimbo la Bunda Mjini, Lucy Msoffe ameshindwa kuithibitishia Mahakama kama alipeleka barua ya kutaarifu wagombea ubunge na vyama vyao, kuhusu kupunguzwa kwa vituo vya kupigia kura kutoka 199 hadi 190.

Pia, Msoffe ambaye ni shahidi namba mbili wa upande wa utetezi, hakuthibitisha kuwapo barua ya kuwataka wagombea kuhudhuria hatua ya kuhesabu kura.

Juzi, kitabu cha kupokelea nyaraka alichokionesha Wakili Tundu Lissu anayemtetea Mbunge wa Jimbo hilo Esther Bulaya, hakikuonesha aliyepokea nyaraka hizo.

Msoffe aliiambia Mahakama kuwa alimtuma mhudumu wa ofisi ya Msimamizi wa Uchaguzi jimboni humo, Masaulu Oktoba 16, mwaka jana kupeleka barua yenye orodha ya vituo 190 na kusainiwa na Katibu wa Wilaya wa CCM.

Hata hivyo kitabu cha kupokelea nyaraka hakikuonesha saini ya Katibu huyo.

Aidha, alidai kuwa hakumbuki siku alipopeleka orodha ya vituo 199 na mwaliko katika ofisi za vyama vya wagombea na kusainiwa na makatibu wa wilaya.

Alitoa madai hayo alipohojiwa na wakili wa waleta maombi, Hajira Mgura aliyemtaka kuionesha Mahakama sehemu iliyotiwa saini na Katibu huyo kwenye kitabu cha kupokelewa nyaraka.

Akiulizwa maswali na Wakili Hajira, Msoffe alidai kuwa hakupata barua kutoka ofisi ya CCM ikionesha jina la wakala wa majumuisho na mgombea.

Shahidi huyo alikiri kwamba kwa mujibu wa sheria, Msimamizi wa Uchaguzi akikamilisha upokeaji wa matokeo kutoka vituoni, ndipo huandika barua ya kutaka wagombea au mawakala kufika kwenye ukumbi wa majumuisho.

Hata hivyo, alikubali kuwa aliandika barua hiyo kabla ya kumaliza kupokea matokeo kutoka vituoni na haikuwa sahihi.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo