Mataka akiri kuomba kukiuka sheria


Grace Gurisha

David Mataka
ALIYEKUWA Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL), David Mataka, amedaiwa kumwandikia barua aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Grey Mgonja aidhinishe maombi ya kukodisha ndege bila kufuata sheria ya ununuzi, hali ambayo iliisababishia Serikali hasara ya dola 772,402.08 za Marekani.

Hayo yalidaiwa jana na Ofisa Mtendaji Mkuu mstaafu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), Ramadhan Mlinga, baada ya Wakili wa Serikali Mkuu, Timon Vitalis kuwasomea washitakiwa maelezo ya awali na kukiri kumwandikia barua Mgonja.

Baada ya kusomewa maelezo hayo, Mlinga alikiri kuwa Februari 27, 2008 Mgonja alimwandikia barua kutaka kujua kama mchakato wa kukodisha ndege unaofanywa na ATCL unafuata sheria za ununuzi, akamjibu Mgonja kuwa hawafuati utaratibu huo.

Ilidaiwa kuwa Machi 12, 2008 Mlinga alimwandikia Mataka kumshauri kuwa amwandikie Mgonja ili apate idhini ya makubaliano na Serikali ya kukodisha ndege bila kufuata sheria hiyo.

Machi 19, 2008 Mataka aliomba idhini hiyo kwa Mgonja, na kusababisha Mgonja naye aandike barua kwa Mlinga ili kupata ushauri, ambapo siku hiyo hiyo naye aliandika barua kwa Mkurugenzi wa Idara ya Uthibitisho wa Mali za Umma wakutane kuzungumza suala hilo.

Vitalis alidai kuwa tarehe hiyo hiyo, Mlinga alimshauri Mgonja kuidhinisha mchakato huo, kwa sababu tayari kulikuwa na makubaliano yaliyokwishafanyika baina ya ATCL na kampuni ya Wallis Trading Inc ya Liberia.

Mataka alikanusha madai yote yalikuwa yakimkabili ya kuisababishia Serikali hasara ya dola hizo, lakini akakiri taarifa zake binafsi.

Kesi hiyo iliahirishwa hadi Novemba 23 ambapo mashahidi wa  upande wa mashitaka watasikilizwa. Mbali na Mlinga na Mataka, mshitakiwa mwingine ni mwanasheria wa PPRA, Bertha Soka.

Washitakiwa hao wanakabiliwa na mashitaka sita yakiwamo ya matumizi mabaya ya madaraka, kughushi na kuisababishia hasara Serikali kupitia ukodishaji wa ndege.

Wakili Vitalis alidai kuwa Oktoba 9, 2007 katika ofisi za ATCL wilayani Ilala, Mataka alitumia vibaya madaraka kwa kusaini mkataba wa ukodishaji ndege A320-214 iliyotengenezwa kwa namba 630 baina ya Wallis Trading Inc na ATCL.

Alidai alifanya hivyo bila kuzingatia Sheria ya Ununuzi wa Umma na taratibu za zabuni kwenye mchakato huo.

Pia, alidai kuwa Oktoba 27, 2007 alitumia vibaya madaraka yake kwa kusaini cheti cha kuruhusu mchakato wa ukodishaji ndege hiyo bila ya kufuata ushauri wa kiufundi na kuisababishia Serikali hasara ya dola 772,402.08 za Marekani zilizolipwa kwa kampuni ya Aeromantenimiento, S. A kama gharama za huduma ya matengenezo.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo