Kesi ya ubunge yavuta wengi Arusha


Seif Mangwangi, Arusha

John Kahyoza
MAMIA ya watu kutoka wilaya ya Longido na jijini hapa jana walifurika kwenye Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, kusikiliza uamuzi wa rufani ya kesi ya ubunge wa jimbo la Longido.

Hata hivyo uamuzi huo ulisogezwa mbele baada ya kudaiwa kuwa wakata rufaa walishindwa kuwajumuisha kwenye kesi hiyo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) na aliyekuwa msimamizi wa uchaguzi jimboni humo.

Majaji wa Mahakama ya Rufani, Jaji Sauda Mjasiri, Mussa Kipenka na Profesa Ibrahim Juma, waliokuwa wanasikiliza rufani hiyo, walitoa uamuzi huo jana, ukisomwa na Msajili wa Mahakama ya Rufani nchini, John Kahyoza

Katika uamuzi huo, waliamua upande wa rufaa uliopinga kutenguliwa matokeo ya ubunge wa Longido, uwaongeze AG na Msimamizi wa Uchaguzi kwa walichodai ni muhimu katika kesi hiyo kazi inayotakiwa kufanyika ndani ya siku 21 ili kuruhusu kuendelea kwa rufani ya msingi.

Msajili Kahyoza akisoma uamuzi wa majaji hao, alisema katika rufani hiyo, Wakili wa wajibu rufaa, Masumbuko Lamwai na Edmund Ndemela waliokuwa wanamtetea aliyekuwa mgombea wa CCM, Dk Steven Kiruswa waliwasilisha hoja, kutaka rufani hiyo, itupwe kwa kuwa waliokata rufani hawajawajumuisha, AG na Msimamizi wa Uchaguzi.

Hata hivyo, mawakili wa aliyekuwa Mbunge wa Longido, Onesmo ole Nangole, Wakili Method Kimomogoro na John Materu, walipinga hoja hiyo kwa maelezo wao tayari waliwapatia AG na Msimamizi Notisi ya kukata rufani na hoja za rufani.

Kimomogoro alisema baada ya kukawabidhi, walitarajia kujumuika kwenye rufaa ya kupinga mteja wao kuvuliwa ubunge, lakini awali walikuwapo na baadaye wakajitoa.

Majaji walisema wameshindwa kuitupilia mbali rufani hiyo, kwa kuwa ina hoja za msingi, lakini wakakubaliana na nusu ya baadhi za hoja za Wakili Lamwai kuwa AG na Msimamizi ni watu muhimu katika kesi hiyo.

Walisema kwa kuwa sababu zote tatu za kutenguliwa matokeo, zilitokana na Msimamizi wa Uchaguzi kushindwa kutimiza wajibu wake, katika rufani alipaswa kushirikishwa.

"Kutoshirikishwa kwa AG na Msimamizi ni kuwanyima haki yao ya msingi kusikilizwa na ndio sababu Mahakama ya Rufani imetumia kifungu cha 111 cha kanuni za Mahakama hiyo, kuagiza waunganishwe katika shauri hilo," alisema Kahyoza.

Majaji waliagiza nyaraka zipelekwa upya katika Mahakama hiyo ndani ya siku 21 zikiwajumuisha maofisa hao na kuhusu gharama za rufani hiyo, zitalipwa baada ya kutolewa uamuzi wa mwisho.

Katika uchaguzi uliopita, Nangole alitangazwa mshindi baada ya kupata kura 20,076 dhidi ya 19,352 za Kiruswa.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo