DCI Diwani adaiwa kuponzwa na pembe za ndovu


Mwandishi Wetu

SIKU moja baada ya Rais John Magufuli kutengua uteuzi wa aliyekuwa Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI), Diwani Athuman, imebainika kwamba uchunguzi dhidi ya ujangili uliofanikisha kukamatwa kwa pembe za ndovu 50 ndiyo sababu ya kutumbuliwa kwake.

Habari za ndani kutoka katika vyanzo mbalimbali zilizolifikia JAMBO LEO zinabainisha kwamba shushushu huyo mkuu alipewa taarifa za kuwepo kwa pembe hizo, lakini alishindwa kutoa ushirikiano kwa wasaidizi wake.

Inaelezwa kwamba kushindwa kwa bosi huyo kutoa ushirikiano kuliwasukuma wasaidizi wake hao ‘kumchoma’ kwa kumpa taarifa mkuu wa nchi (Rais Magufuli).

Inadaiwa kwamba kwa mujibu wa taratibu za utendaji kazi za kipelelezi, DCI ndiye anayetakiwa kutoa maelekezo katika matukio kama hayo ya uharamia wa pembe za ndovu, lakini katika tukio hilo Diwani alionesha udhaifu.

Chanzo chetu cha habari kinadai kuwa baada ya wasaidizi wake kutoa taarifa za kuwepo kwa mzigo huo haramu naye kutoonyesha ushirikiano waliwasiliana na wenzao wa Idara ya Usalama wa Taifa, ndipo taarifa zikafika kwa Rais.

“Baada ya taarifa hizo kufika, Rais alitoa maelekezo kwa mashushu hao kuendelea na mchakato ili waweze kuwakamata majangili hao, huku DCI Diwani akiwa hajui nini kinaendelea,” kilieleza chanzo hicho.

Kiliongeza: “Hapa DCI amezungukwa, suala hili tunachojua aliambiwa lakini akashindwa kuchukua uamuzi. Si unajua biashara hizi ni za wakubwa, wakati mwingine unabaki kama zuzu, hizi kazi ni ngumu sana ila nyie mnatulaumu sisi watenda kazi.”

Alisema watu wanaweza kuona kama DCI ni mzembe lakini ni vyema kutambua kwamba kupambana na biashara hiyo ni lazima kujitoa mhanga kwani kundi hilo lina nguvu ya kila kitu.

Mtoa taarifa huyo alisema dhana kuwa Diwani ameshindwa kuendana na kasi ya Rais Magufuli haina uhusiano na tukio la kutumbuliwa kwake kwani yeye ni moja wa viongozi wa Jeshi la Polisi aliyekuwa akifanya kazi kwa uadilifu na misingi ya kazi.

Alisema hata suala hilo la pembe za ndovu alikuwa amejipanga kupata matokeo chanya, ingawa amekumbwa na bahati mbaya.

Diwani ameondolewa katika nafasi hiyo akiwa amefanya kazi kwa takribani mwaka mmoja na miezi mitano, baada ya kuteuliwa Mei, mwaka jana na Rais mstaafu wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete.

Alipoteuliwa kushika wadhifa huo aliweka bayana kuwa matarajio yake ni pamoja na kuona Tanzania inaendelea kuwa na amani na usalama.

Kabla ya uteuzi huo, Diwani alikuwa Kaimu Kamishna wa Kamisheni ya Intelijensia ya Jinai na alipoteuliwa kuwa DCI, nafasi hiyo ilichukuliwa na Naibu Kamishna wa Polisi (DCP), Valentino Mlowola ambaye kwa sasa ni Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa.

Kabla ya hapo, mwaka 2012, Diwani alihamishiwa mkoani Mbeya kuchukua nafasi ya Kamanda Advocate Nyombi na kuwa kamanda wa polisi wa mkoa huo.

Kabla hajawa RPC, aliwahi kushika nafasi nyingine za kiutendaji na kiutawala kama mlinzi wa IGP mstaafu Omari Mahita, Kaimu Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Mbeya na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga.

Juzi kupitia Katibu Mkuu Kiongozi Mhandisi John Kijazi alitoa taarifa ya kutengua uteuzi wa Athuman huku kukiwa hakuna sababu ya utenguaji huo iliyoanishwa.

Aidha, taarifa hiyo ilieleza kuwa DCI Athuman atapangiwa kazi nyingine na kuwa uteuzi wa DCI mwingine atatangazwa baadaye.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo