Samia apiga marufuku uharibifu mazingira


Suleiman Msuya

Makamu wa Rais, Samia Suluhu
MAKAMU wa Rais, Samia Suluhu Hassan, amepiga marufuku uharibifu wa mazingira unaendelea katika maeneo mbalimbali nchini, akisema unaweza kusababisha nchi kugeuka jangwa.

Samia alitoa kauli hiyo jana alipozungumza na waandishi wa habari baada ya kufungua mkutano wa kimataifa kuhusu mabadiliko ya tabianchi unaokutanisha wanasayansi, watafiti na wadau wa mazingira chini ya usimamizi wa Kigoda cha Mwalimu Nyerere cha Mazingira na Mabadiliko ya Tabianchi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

Alisema jukumu la kuhifadhi mazingira si la Serikali peke yake bali ni kila mwananchi na wadau wa mazingira kwa ujumla, hivyo wananchi ni muhimu kwa umoja wao wakaongeza jitihada za kupanda miti katika maeneo yao ili kukabiliana na hali uharibifu wa mazingira.

“Uharibifu wa mazingira usimame leo na marekebisho ya uharibifu tulioufanya uanze leo na hili ni jukumu la kila Mtanzania,” alisema.

Aidha, Makamu wa Rais alitoa mwito maalumu kwa viongozi wa ngazi zote nchini kuchukua hatua za kulinda na kuhifadhi vyanzo vya maji katika maeneo yao ili visitoweke.

Alisema mabadiliko ya tabianchi yameanza kuleta athari duniani, hivyo jitihada za makusudi zinahitajika ili kuhakikisha changamoto zinazojitokeza sasa zinakabiliwa ipasavyo.

Mkurugenzi wa Kituo cha Mafunzo ya Mabadiliko ya Tabianchi wa UDSM, Profesa Pius Yanda alisema mkutano huo wa siku tano utakuwa na jukumu la kujadili kwa kina, namna bora ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo