Dawa bandia zazua balaa


* Za malaria zachangia asilimia 45 ya vifo
* Watengenezaji wafananishwa na magaidi

Leon Bahati

VIFO vya watu 200,000 hadi 450, 000 kati ya milioni moja kutokana na malaria katika nchi zinazoendelea, Tanzania ikiwamo, hutokana na matumizi ya dawa bandia.

Hayo yamo katika utafiti uliofanyika nchini na taarifa yake kutolewa Mei mwaka huu na jopo la watafiti.

Watafiti hao ni pamoja na Linus Mhando, Mary Jande, Anthony Liwa, Stanley Mwita na Karol Marwa wa Chuo Kikuu cha Afya cha Kanisa Katoliki mkoani Mwanza.

Watafiti hao wamebainisha kuwa hali hiyo inatokana na kusambaa kwa dawa bandia za malaria na magonjwa mengine kwenye maeneo mengi nchini.

“Tunachoshauri ni wananchi kupewa elimu ya kutambua dawa bandia ikiwa ni pamoja na kuweka mfumo utakaowakatisha tamaa watengenezaji wa dawa hizo,” inaeleza sehemu ya hitimisho la utafiti huo.

Kwa mujibu wa utafiti huo, kati ya watu milioni moja wanaokufa kwa malaria 200,000 hadi 450,000 hufa kutokana na dawa bandia.

Aidha, watafiti hao walieleza kuwa kwa mujibu wa utafiti katika nchi zinazoendelea Tanzania ikiwamo, asilimia 10 hadi 15 ya dawa zinazouzwa humo ni bandia.

Kwa sababu hiyo, kwenye ripoti yao walipendekeza moja ya njia za kukabili watengenezaji dawa bandia ni kuwa na sheria zinazoidhinisha adhabu kali.

Watafiti hao walipendekeza moja ya kanuni hizo iwe ni kuadhibu kwa mujibu wa sheria ya ugaidi inayoonesha mauaji ya makusudi.

Kuhusu sababu za kupendekeza sheria kali zitumike kuadhibu wahusika wa dawa bandia, watafiti hao walieleza ni kutokana na wanaotengeneza dawa hizo kufanya hivyo huku wakijua zitakuwa hazitibu bali kuua.

Ripoti ya watafiti hao inaonesha kwamba utafiti mbalimbali duniani unabainisha watengenezaji wa dawa bandia kuzitengeneza kwa wingi    na kuingizwa kwenye soko la Afrika.

Sababu kuu waliieleza kuwa ni kutokana na asilimia 90 ya watu milioni tatu wanaougua malaria duniani kuwa Afrika.

Walitoa mfano wa Uganda, ambako asilimia 37 ya dawa bandia ya artemisinin, ambayo ni maarufu zaidi nchini humo imekuwa ikiuzwa kwenye maduka mengi ya rejareja.

“Tanzania kuwa miongoni mwa nchi zinazoendelea haiwezi kamwe kujinasua kwenye janga hilo la dawa bandia,” inaeleza sehemu ya ripoti ya utafiti huo, lakini ikisisitiza kuwa mikakati makini ndiyo itakayozuia dawa hizo kuingia au kutengenezwa nchini.

Kuhusu tafsiri ya dawa bandia, taarifa hiyo ya utafiti ilieleza kuwa zipo dawa za aina nyingi lakini zimegawanyika katika makundi matatu.

Walitaja kundi la kwanza kuwa ni la dawa zenye upungufu wa viambata.

“Kwa mfano; kama dawa ina viambata vitatu, kimoja au viwili hukosekana, hivyo tiba yake kutokuwa kamilifu,” ilieleza sehemu ya utafiti.

Aina ya pili, ilielezwa ni dawa zenye viambata vyote, lakini kuwa kwa kiwango hafifu, hivyo kushindwa kufanya kazi ya tiba kulingana na viwango vya kitaalamu.

Watafiti hao walilielezea kundi la tatu, kuwa ni dawa iliyotengenezwa vizuri, lakini ufungaji wake kutokidhi viwango au kufungwa katika makasha yasiyo sahihi.

Kwa mujibu wa watafiti hao, utafiti uliofanywa na Shirika la Afya Duniani (WHO) mwaka 1999, ulipendekeza kuwapo mkakakati makini wa kuwezesha watu kuzitambua dawa bandia.

Hata hivyo, walipofanya uchunguzi nchini kuona kama wananchi wana ufahamu kuhusu dawa bandia, ilionekana karibu nusu hawajui viashiria vya dawa bandia.

Utafiti huo unaonesha kuwa kati ya watu 293 waliochunguzwa, matokeo yalionesha watu 163 sawa na asilimia 55.6 walikuwa na uelewa, lakini 130 sawa na asilimia 44.4 hawakuwa na elimu hiyo.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo