Mkurugenzi Wilaya kortini kwa kutishia kuua trafiki


Warioba Igombe, Morogoro

JESHI la Polisi mkoani hapa limemkamata na kumfikisha mahakamani Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mkinga (DED) mkoani Tanga, Emmanuel Barnaba (41) kwa tuhuma ya kumtishia kifo askari wa kikosi cha usalama barabarani.

Akithibitisha jana kutokea kwa tukio hilo, Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Ulrich Matei alisema tukio hilo lilitokea Jumamosi maeneo ya Mkambarani baada ya askari Koplo Tutindaga kumwamuru DED kusimama.

Kamanda Matei alisema baada ya mtuhumiwa kusimamisha gari  aina ya Prado, ilibainika kuwa alikuwa anaendesha gari hilo kwa mwendo kasi ikiwa ni pamoja na kutokuwa na leseni.

“Baada ya askari wa kikosi cha usalama barabarani kulisimamisha gari hilo, dereva alikutwa na makosa mengi ikiwa ni pamoja na kuendesha gari kwa mwendo kasi lakini pia kutokuwa na leseni,” alisema Kamanda Matei.

Baada ya askari huyo kubaini makosa hayo, mtuhumiwa alisema hakuwa na fedha za kulipa faini kwa kuwa alikuwa anaendesha gari la Serikali.

Kwa maelezo hayo, ndipo alipomwamuru DED huyo kwenda kituo cha Polisi cha Kingolwira, lakini wakiwa njiani mtuhumiwa alitoa bastola na kumwamuru askari huyo kushuka vinginevyo atamuua.

Inadaiwa kuwa baada ya askari kuona ametishiwa kuuawa, alishuka na kumwacha mtuhumiwa aendelee na safari yake na yeye kufanya wawasiliano na askari wa kituo cha Mikese ambao walimtia nguvuni.

Baada ya Polisi kumkamata mtuhumiwa huyo aliyekuwa anatoka Morogoro kwenda Dar es Salaam walimfikisha kituo kikuu cha Polisi Morogoro na baadaye mahakamani.

Mahakamani mbele ya Hakimu Mkazi Agripina Kimaze, Mwendesha Mashitaka, Sandy Hyela alidai kuwa mtuhumiwa anashitakiwa kwa tuhuma mbili, kutishia kuua kwa silaha la kuvunja sheria za usalama barabarani.

Katika tuhuma ya pili mtuhumiwa anadaiwa kuendesha bila leseni, kukosa bima, mwendo kasi, kukaidi amri halali ya askari wa usalama barabarani na kusimamisha gari katikati ya barabara bila kujali watumiaji wengine.

Baada ya kusomewa mashitaka, mtuhumiwa alikana na  Hakimu Kimaze kusema dhamana kwa mtuhumia iko wazi na ndipo ndugu na jamaa walipomdhamini baada ya kukidhi na kesi hiyo itasikilizwa Oktoba 30.

Hata hivyo wakati anatoka mahakamani hapo ndugu na jamaa zake waliokuwa mahakamani hapo walimficha  ili asionekane kwa waandishi wa habari na kumpiga picha na kisha kumpandisha kwenye gari dogo namba T 830 ARP.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo