Aliyetobolewa macho kuingiza Sh. milioni moja kila wiki


Charles James na Badrudin Yahaya


SIKU moja baada ya mkazi wa Dar
es Salaam, Said Mrisho aliyetobolewa macho kukabidhiwa msaada wa fedha na ahadi ya vitega uchumi, wafanyabiashara wameeleza kuwa akitumia vizuri msaada huo, atajipatia Sh milioni moja kila wiki.

Mrisho aliyetobolewa macho kwa visu Septemba 6 na mtu anayedaiwa kuwa Henjewele Salum ‘Scorpion’ (34), juzi alipewa msaada wa Sh milioni 12, pikipiki tano, bajaji mbili na ahadi ya kununuliwa nyumba.

Wakizungumza na waandishi wa gazeti hili katika nyakati tofauti, wafanyabiashara wa saluni za kunyoa nywele, pikipiki za abiria na bajaji, walitoa ushauri ambao walidai ukifuatwa, kijana huyo atajitegemea kwa kipato hicho.

Bajaji

Wafanyabiashara wa bajaji walisema hesabu ya chombo hicho kibiashara ni Sh 15,000 kwa siku, hivyo Mrisho kwa kila moja atakuwa anaingiza Sh 105,000 kwa wiki sawa na Sh 210,000 kwa bajaji mbili kwa wiki.

Dereva na mmiliki wa bajaji anayefanya shughuli zake kwenye kituo cha Sinza, Emmanuel Dito alisema kwa hali aliyonayo Mrisho, ni vema asitoe vyombo vyake kwa mkataba, badala yake awape madereva watakaomletea hesabu ya siku, ili vyombo hivyo vimlinde kwa muda mrefu.

“Mimi namshauri kijana mwenzangu atafutiwe wasimamizi wa uhakika watakaokuwa waaminifu, ili adumu na vyombo vyake kwa muda mrefu lakini pia ahakikishiwe anakatiwa bima kubwa kwa vyombo vyake vyote kwa ajili ya kuvilinda zaidi,” alisema.

Loti Sadiki, dereva wa bajaji, alisema kazi hiyo kwa upande mwingine ni ngumu kwa kuwa kuna baadhi ya maeneo kama mjini hawaruhusiwi kuingia na kutokana na usalama, mara nyingine wanalazimika kulaza vyombo mapema na kusababisha hesabu kuwa ngumu kutimia.

Bodaboda

Madereva na wamiliki wa pikipiki za biashara maarufu kama bodaboda, walisema kwa siku pikipiki moja inaingiza Sh 7,000 hivyo kwa siku sita itakuwa ni Sh 42,000 na kwa idadi ya pikipiki tano alizokabidhiwa ataingiza Sh 210,000 kwa wiki.

Said Kitindi, dereva wa bodaboda Mwenge, alishauri Mrisho asikubali kutoa pikipiki kwa madereva kwa mikataba, kwa maelezo kuwa mfumo huo mara nyingi unatumiwa na watu wenye biashara zao.

Kwa mujibu wa Kitindi, wanaotumia mfumo wa mkataba fedha za vyombo hivyo huingia katika mzunguko wa kila siku wa biashara zingine, lakini kwa hali aliyonayo Mrisho, ni vema atunze vyombo hivyo na achukue hesabu kila siku kwa muda mrefu ili vimsaidie.

Dereva mwingine wa bodaboda, Zuberi Omary hakuwa mbali kimawazo na wenzake, akipendekeza Mrisho apokee hesabu yake kwa siku au wiki, ili ajikimu kimaisha kwa muda mrefu, tofauti na mkataba ambao ukifika mwisho, atapata ugumu kiasi wa kupata pikipiki nyingine.

Mafundi

Mafundi wa bodaboda na bajaji, walisema vyombo hivyo vinavyotumika kila siku huhitaji matengenezo ya hapa na pale, hivyo ili vifanye kazi kwa muda mrefu, ni lazima vipate matengenezo hayo.

Mohamed Yassir, fundi wa bajaji na pikikipi, alisema matengenezo ya bodaboda ni mara moja kwa wiki, ambapo gharama zake hazizidi Sh 10,000 na kwa upande wa bajaji, ni mara mbili kwa mwezi na gharama yake ni Sh 15,000.

Saluni
Kuhusu biashara aliyozoea ya kunyoa nywele, Mrisho alishauriwa kama akiwekeza kwenye biashara hiyo, ana uwezekano wa kuanzisha saluni za kisasa mbili na kuvuna kipato kizuri kwa wiki.

Mmoja wa vinyozi wa Gongo la Mboto, Hamad Chande alisema saluni moja huwa na viti vinne na kila kiti na kinyozi wake atakayetakiwa kumlipa Sh 90,000 kwa wiki Sinza na Sh 50,000 kwa wiki Buguruni.

Kwa mujibu wa Chande, kwa saluni za Sh 90,000 kwa kiti, Mrisho anaweza kujipatia Sh 360,000 kwa wiki na kwa Sh 50,000, atajipatia Sh 200,000.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo