*Ukame wakumba maeneo mbalimbali
*Vyakula
vyapanda bei, wanyama wafa
Waandishi
Wetu
NJAA na ukame sasa ni dhahiri nchini.
Hiyo ndio hali halisi iliyoikumba mikoa kadhaa iliyosababisha
ongezeko la bei za vyakula.
Uchunguzi uliofanywa na JAMBOLEO
umebaini kwamba wananchi wa mikoa ya Mara, Kilimanjaro, Pwani, Morogoro,
Simiyu, Shinyanga, Singida, Tabora, Arusha, Manyara na Tanga wanalia ukame
kukithiri kila kukicha.
Taarifa zinaonesha kwamba wilayani Bunda,
Mara, wananchi wanakabiliwa na upungufu mkubwa wa chakula huku bei ikipanda kwa
kasi.
Uchunguzi kwenye maeneo mbalimbali na
kwenye masoko wilayani humo, ulibaini kuwa bei ya chakula ilipanda kuanzia
Agosti na Septemba mwaka jana.
Ulionesha bei ya chakula kupanda kutoka Sh
14,500 kwa debe la mahindi hadi Sh. 20,000; mtama kutoka Sh 10,000 hadi Sh
17,500; unga wa muhogo kutoka Sh 12,500 hadi Sh 17,500 na ulezi unauzwa Sh
30,000 kwa debe.
Baadhi ya wafanyabiashara wa nafaka kwenye
soko kuu la mjini humo na mji mdogo wa Kibara jimboni Mwibara, walisema bei ya
chakula imepanda kutokana na upungufu mkubwa wa nafaka.
Mkazi wa eneo hilo, Esther Samson alisema
hali hiyo ilisababishwa na mvua kutonyesha wilayani humo kwa kipindi kirefu na
kusababisha mazao yaliyolimwa kunyauka.
Esther alisema wamekuwa wakiuza chakula wanachopata
kutoka mikoa jirani kwa bei ya juu ili kurudisha mtaji na kupata faida kidogo.
“Hali ya chakula kwenye soko letu ni
mbaya maana kimepanda kutokana na sisi tunavyouziwa kwa bei ya juu. Na hii hali
tuseme ilianza Agosti na Septemba mwaka jana. Sasa hivi gunia la mahindi tunanunua
kati ya Sh 110,000 na Sh 120,000,” alisema.
Mkazi wa kijiji cha Changuge, Juma
Mabyora alisema wanakabiliwa na njaa kubwa na hali hiyo inatokana na ukame na
pia baadhi ya mazao mashambani yalishambuliwa na tembo kutoka Hifadhi ya Serengeti.
“Jamani tusidanganyane, hali ya
njaa katika wilaya yetu iko wazi, baadhi ya familia zinakula mlo mmoja, tena zingine
zinashinda na kulala na njaa. Kwanza hata fedha hazionekani, yaani hali ni
mbaya sana. Sasa angalia eti kilo tano za mahindi tunauziwa Sh 4,000,” alisema
na kuongeza:
“Tunaomba
Serikali ituletee chakula hata cha bei nafuu, maana hali ni mbaya sana katika
maeneo yetu.”
Diwani wa Bunda Mjini, Joash Kunaga na Diwani
wa Bunda Stoo, Daud Chiruma walisema wakazi wa kata zao wanakabiliwa na
upungufu mkubwa wa chakula na bei ya chakula ambacho kimekuwa kikipatikana iko
juu, hali ambayo inasababisha wengine kushindwa kununua.
Diwani wa Nyamuswa, Fyeka Sumera naye
kama wenzake alisema wakazi wa kata yake wanakabiliwa na upungufu mkubwa wa
chakula
Kilimanjaro
Wananchi wa Wilaya ya Siha mkoani
Kilimanjaro wamekumbwa na hofu kubwa ya kukumbwa na njaa
muda wowote kutokana na ukame uliokithiri wilayani humo kutokana na
mazao yao kukaukia mashambani, hivyo kuambulia mabua.
Walisema tatizo la chakula linaonekana
kuwa kubwa kutokana na ukame ambao ni mkubwa wilayani humo kwani tangu mwaka
jana hawakupata chakula cha kutosha.
Mkazi wa wilaya hiyo, Andrew Laizer
alisema kwa sasa hali ni mbaya kwani mazao waliyopanda yalikaukia mashambani.
Kwa hofu hiyo kubwa ya kukumbwa na njaa
waliiomba Serikali kuchukua hatua ya kuwanusuru na baa hilo ambalo litawasababisha
kula mizizi.
Mbunge wa Siha, Godwin Molel akizungumzia
upatikanaji wa chakula wilayani humo, alisema ni mbaya kwani kwa mwaka jana
chakula hakikupatikana, hivyo aliahidi kufikisha suala hilo ngazi husika, ili
wananchi wanusuriwe na baa hilo.
Alisema ameshirikisha madiwani wa wilaya
hiyo, kuangalia namna ya kukabiliana nalo lakini atahakikisha analifikisha ngazi
husika kukabiliana na hali hiyo ili kunusuru wananchi hao.
"Kweli baa la njaa wilayani hapa lipo
na katika kunusuru nina mpango wa kwenda kuonana na Waziri Mkuu kumweleza hali
halisi ilivyo, ili waone jinsi ya kunusuru wananchi hawa ambao tayari wana hofu
ya kukumbwa na njaa, ili serikali iwasaidie chakula," alisema Molel.
Pwani,
Moro
Hali hiyo imeonekana pia Pwani na
Morogoro ambako pamoja na wananchi kukosa chakula hata mifugo imekuwa ikifa
kila siku huku bei za vyakula zikipanda.
Mfugaji Solengei Saitoti wa Morogoro alisema
ameshapoteza mifugo zaidi ya 50 huku
kukiwa hakuna dalili za mvua kunyesha ili kuikoa.
Hali ya Hewa
Ikizungumzia
hali ya mvua nchini, Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA)
ilisema mvua itaendelea kunyesha maeneo yanayopata msimu mmoja wa mvua kwa
mwaka kati ya Januari na Februari.
Meneja Ofisi Kuu ya Utabiri wa Hali ya
Hewa, Samwel Mbuya alisema kwa maeneo yanayopata misimu miwili ya mvua, mvua za
vuli zilizokuwa zinaanzia Novemba hadi Desemba mwaka jana umeshapita.
Mbuya alisema maeneo ya Kanda ya
Magharibi na Nyanda za Juu Kusini Magharibi zenye mikoa ya Tabora, Katavi, Kigoma,
Rukwa, Songwe, Mbeya, Njombe na Iringa, yanatarajiwa kupata mvua za kiwango cha
wastani katika kipindi hiki.
Aidha, alieleza kuwa Kanda ya Kati yenye
mikoa ya Singida na Dodoma, inatarajiwa kuwa na mvua za chini ya kiwango, huku
Kanda ya Kusini yenye mikoa ya Ruvuma, Mtwara na Lindi itakuwa na mvua za
wastani hadi chini ya wastani.
Mbuya alisema maeneo ya Kaskazini mwa nchi
yenye mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Tanga, Kilimanjaro, Arusha, Morogoro,
Simiyu na Manyara ambayo huwa na misimu miwili ya mvua kwa mwaka, msimu wa vuli
umemalizika.
Aliongeza kuwa mikoa ya Kanda ya Ziwa
pia itaendelea kupata mvua za kawaida.
Aliwataka wananchi kuendelea kufuatilia
taarifa za hali ya hewa, ili kujua mwenendo wa mvua na pia ushauri wa wataalamu katika
masuala hayo, ambapo alibainisha kuwa kufanya
hivyo kutawasaidia kwenye shughuli za kiuchumi na kilimo.
0 comments:
Post a Comment