Mwandishi Wetu
Kassim Majaliwa |
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, ametangaza kukabidhi pikipiki 200
zenye thamani ya sh. milioni 400 kwa vijana 200 wa Jiji la Arusha waliokuwa
wakiendesha pikipiki za watu binafsi zisizo na tija, ili kuweza kuwakwamua
kiuchumi na kujitegemea kwa mapato.
Majaliwa amegawa pikipiki hizo ambazo zimechangwa na wadau
mbalimbali wa maendeleo mkoani Arusha baada ya Mkuu wa Mkoa huo. Mrisho Gambo
kubuni mpango huo kwa lengo la kuwawezesha vijana kupata pikipiki bila riba
wala dhamana.
Waziri Mkuu alikabidhi pikipiki hizo juzi baada ya kumaliza
kuhutubia maelfu ya wananchi waliohudhuria katika mkutano wa hadhara kwenye
Uwanja wa Sheikh Amri Abeid.
“Nawataka vijana mhakikishe mnakuwa waaminifu kwa kufanya kazi kwa
bidii ili pikipiki ziweze kuwasaidia kuwainua kipato,” alisema Majaliwa.
Katika hafla hiyo, Waziri Mkuu alisema mwananchi yeyote hata kama
si mtumishi wa umma ana wajibu wa kuiheshimu Serikali na kuitumikia, akiwataka
vijana hao pia kuwa waadilifu.
“Serikali ya awamu ya tano imeanza kazi na moja kati ya majukumu
yetu ni kuboresha nidhamu ndani na nje ya Serikali hivyo ni lazima ipate
heshima yake.”
“Tumeamua kuwatumikia. Tumeamua kuwahudumia Watanzania wote bila
ya kujali itikadi zao za kisiasa na kidini na Mheshimiwa Rais anataka kuona
wananchi wake akifurahia Serikali yao,” alisema.
Kwa upande wake Gambo alisema pikipiki hizo zilizokabidhiwa kwa
vijana hao zimetolewa zikiwa na bima kubwa huku kila Kata ikitoa vijana wanane.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu alisema zaidi ya Sh. bilioni
800 zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo mkoani Arusha.
Majaliwa ambaye yuko mkoani Arusha kwa ziara ya kikazi alisema
kati ya fedha hizo sh. bilioni 476 zitatumika katika ujenzi wa miradi wa maji
ili kumaliza kero hiyo. “Mkoa wa Arusha unakabiliwa na changamoto kubwa ya
upatikanaji wa maji safi na salama, hivyo fedha hizo zinalenga kumaliza tatizo
hilo ambalo limechangiwa na uharibifu wa mazingira,” alisema.
Alisema kiasi kingine cha Sh. bilioni 264 kilitolewa ili
kuimarisha upatikanaji wa umeme wa uhakika katika mkoa huo.
0 comments:
Post a Comment