Suleiman Msuya
WAKATI Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Festo Kiswaga, akitangaza
kukataza chama cha Chadema, kuzindua Oporesheni Kata Funua iliyopangwa
kuzinduliwa leo, Kamanda wa Polisi mkoa huo, Onesmo Lyanga, amepata kigugumizi
kuzungumzia operesheni hiyo na kumtupia mpira mkuu wa mkoa huo huku chama hicho
kikisisitiza kuuzindua leo.
Jana Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Festo Kiswaga, ambaye pia ni
Mkuu wa Wilaya ya Bariadi alikaririwa na vyombo vya habari akizuia Chadema
kufanya uzinduzi huo.
Wakati Kiswaga akitoa zuio hilo, jana Kamanda Lyanga alisema hawezi
kujibu katazohilo huku akimtaka mwandishi azungumze na kaimu mkuu wa mkoa huyo.
“Siwezi kuzungumzia kauli ya mkuu wa mkoa, kama unataka mpigie
yeye kwani ndiye amesema, si mimi niliyesema,” alisema.
Hata alipoambiwa kuwa utekelezaji wa agizo la katazo la Mkuu wa
Mkoa utafanywa na ofisi yake, kamanda huyo alisisitiza kuwa hana cha kuzungumza
na kukata simu.
Hata hivyo, Naibu Katibu Mkuu Chadema Zanzibar, Salim Mwalimu
ambaye tayari yupo Simiyu kwa uzinduzi huo alisema anachokiona ni kuwepo
viongozi wanaotafuta umaarufu kupitia chama chao na viongozi wake.
Mwalimu alisema ni jambo la kushangaza kuona watu wanakataza
mikutano ya ndani na wengine wanaruhusu jambo linaloonesha kuwa wapo ambao
wanatafuta umaarufu kupitia wao.
“Unajua kuna watu wakisikia Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa
anafika mahali wanataka kutumia jina lake kutafuta uamaarufu ila sisi
tunawapuuza kwani hawana jipya,” alisema.
Alisema wao wanajua taratibu zote za kufanya mikutano na wameshazifuata
hivyo hawasumbuliwi na watu ambao wanatafuta umaarufu kupitia migongo yao na
viongozi wao.
Mwalimu alisema ni aibu kuona viongozi wanatoa kauli za uongo bila
ushahidi jambo ambalo linazalilisha nafasi zao na jamii kwa ujumla.
“Kama anasema wapeta taarifa za kuwepo kwa vurugu kwanini hawataji
aliyewaambia na kuonesha ushahidi wanatupotezea muda,” alisema.
Mwalimu alisema ni vema Serikali ikafanya kazi zake kwa kufuata
taratibu kwani wao hawana mpango wowote wa kuingiza nchi katika machafuko au
fujo kama inavyosemwa na mkuu huyo wa mkoa.
Katika katazo lake kaimu mkuu huyo wa mkoa alisema wamepata
taarifa kuwa mkutano huo wa uzinduzi operesheni kata funua utakuwa na vurugu
jambo ambalo hawezi kuruhusu litokee. Alisema kupitia operesheni hiyo Chadema
inatarajia kuwataka wananchi wafanye migomo hali ambayo itasimamisha shughuli za
wananchi.
Kiswaga aliitaka Chadema kuacha wananchi wafanye shughuli za
uzalishaji na kuachana na dhana ya kufanya maandamano kila kukicha.
0 comments:
Post a Comment