Unyanyasaji kijinsia waongezeka Ilala


Salha Mohamed

Kamanda Salum Hamduni
KESI za unyanyasaji wa kijinsia na ukatili dhidi ya watoto na wanawake zimeripotiwa kuongezeka kwa asilimia 42.3 mwaka huu wilayani Ilala.

Hayo yalibainishwa Dar es Salaam Jumatano na Jeshi la Polisi Mkoa wa wa Ilala ikiwa ni kuelekea maadhimisho ya siku 16 ya kupinga ukatili wa kijinsia yanayotarajiwa kufanyika Desemba 5.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ilala, Salum Hamduni, alisema ongezeko hilo linatokana na kupata taarifa za siri za unyanyasaji wa kijinsia kutoka kwa raia wema kama kutelekeza familia, migogoro ya ndoa ambapo waathirika wakuu ni wanawake na watoto.

Alisema tayari Polisi imetoa rufaa kwa kesi 70 kati ya Januari na Septemba kwenda Manispaa kwa Mkurugenzi Kitengo cha Ustawi wa Jamii huku rufaa 52 zikitolewa katika Januari hadi Desemba mwaka jana.

"Makosa ya jinai yanayojitokeza kila wakati ni ulawiti, ubakaji, vipigo, shambulio la aibu, shambulio la kudhuru mwili, lugha ya matusi na shambulio la kawaida," alisema.

Alisema katika maadhimisho hayo, watashirikiana na Shirika la Kimataifa la Wanawake katiak Sheria na Maendeleo Afrika (WilDAF), kuandaa maandamano ya amani yatakayoanzia Tazara hadi shule ya msingi Vingunguti.

"Lengo la maadhimisho hayo ni kuenzi siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia ambapo kampeni kabambe ya kimataifa inayoongozwa na kituo cha kimataifa cha wanawake katika uongozi kilitenga siku ya kutetea haki za wanawake tangu Novemba 25, 1991," alisema.

Kamanda Hamduni alisema chimbuko la kupinga ukatili wa kijinsia na mauaji lilianza baada ya tukio la mauaji ya dada wa Mirabelle yaliyofanyika Dominica katika visiwa vya Karibeani mwaka 1960.

"Siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia zimekuwa zikitumiwa na  Polisi na wadau duniani kama mbinu mahsusi za kutoa mwito kwa jamii kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake kwa kuelimisha jamiii kuhusu ukatili wa kijinsia na kutoa taarifa kwenye vituo vya Polisi ili kulinda wanawake na watoto dhidi ya ukatili,” alisema.

Alisema Polisi imekuwa ikitumika kwenye maadhimisho hayo kama chombo cha kupaza sauti ili wadau watekeleze wajibu wao katika kupiga vita na ukatili dhidi ya wanawake.

"Mkoa wa Ilala katika kupambana na ukatili wa kijinsia na watoto umefungua madawati tisa katika vituo vikubwa vya Polisi na vya kati yanayotoa huduma kwa jamii dhidi ya vitendo vya ukatili na unyanyasaji katika vituo vya Ilala, Wilaya ya Kati, Kariakoo, Stakishari, Buguruni, Pangani, Tabata, Selander Bridge na Vingunguti," alisema.

Alisema mgeni rasmi katika maandamano hayo atakuwa ni Mkuu wa Wilaya, Sophia Mjema huku akiwataka wananchi kujitokeza siku hiyo muhimu na ya thamani kwao kwani ulinzi na usalama utakuwa wa kutosha.

Aidha, Hamduni aliomba wananchi hasa wanawake na watoto kuendelea kutoa taarifa za unyanyasaji na udhalilishaji katika vituo vya Polisi ili kutokomeza ukatili huo.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo