Dk Shein: ICC haina uwezo kuhoji Uchaguzi Zanzibar


Peter Akaro

Dk. Ali Mohamed Shei
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi (SMZ), Dk. Ali Mohamed Shein amesema Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC), haina uwezo wa kuhoji uchaguzi wa visiwa hivyo.

Aliwataka wananchi wa Kisiwa cha Pemba kupuuza taarifa kwamba kuna Serikali nyingine itaingia madarakani visiwni humo, badala yake waendelee kufanya kazi kwa bidii kwa kushirikiana na SMZ.

Taarifa ya Ikulu ya Zanzibar iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari ilisema Dk. Shein amewaambia wananchi kisiwani humo kwamba Serikali anayoiongoza iko madarakani kwa mujibu wa Katiba na inaendelea kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM hadi mwaka 2020.

“Wanaisingizia ICC, wanadanganya tu haina uwezo huo wa kuhoji uchaguzi wa Zanzibar ulioendeshwa kwa mujibu wa Katiba yake,” alisema Dk. Shein ambaye yuko kisiwani Pemba kwa ziara ya kikazi.

Dk Shein alionyesha kukerwa na uzushi huo. Aliwakumbusha wanasiasa wanaoeneza uvumi wa kuingia madarakani kwa Serikali nyingine akisema kiongozi anayetaka ushindi ni lazima ashiriki uchaguzi, achaguliwe na wananchi na atangazwe na Tume ya Uchaguzi kuwa ni mshindi.

“Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ipo na mimi ndie Rais. Ni serikali halali kwa mujibu wa Katiba ya mwaka 1984,” alisema.

Aliwahakikishia wananchi hao kwamba hakuna nchi wala taasisi ya ndani au ya nje inayoweza kuiondoa Serikali iliyopo sasa, wala hakuna wa kuhoji uhalali na uwepo wake.

“Hakuna nchi inayoapisha Rais mara mbili, mimi sina wasiwasi na Serikali yenu haina wasiwasi na tuko hapa kuwatumikia ili kuendeleza nchi yetu, maneno haya yanawapotezea muda wenu tu,” alisema na kufafanua:

“Serikali hii ni ya wananchi waliyoichagua na wasioichagua, waliopiga kura na wasiopiga kura. Wapo wanayoitaka na wasiyoitaka, wote hao wanafanya kwa hiari yao, lakini mwisho wa yote kwa kuwa tayari imewekwa madarakani na wananchi wenyewe kupitia uchaguzi ulioendeshwa kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar hawana budi kuitii.” 

Alibainisha kuwa ni tamaa za baadhi ya wanasiasa waliowashawishi baadhi ya watu wasishiriki katika uchaguzi wa marudio ambao uliitishwa kwa mujibu wa Katiba lakini sasa baada ya kuona waliyoyatarajia hawakuyapata sasa wanawazubaisha wananchi kwa kupita mitaani na maneno yasiyo na msingi.

Dk. Shein aliyewasili kisiwani Pemba juzi na kuzungumza na wananchi wa Mji wa Chake Chake wakati wa uzinduzi wa jengo la Mahakama Kuu na wananchi wa Kengeja wakati alipozindua dakhalia ya wasichana ya skuli ya sekondari ya ufundi Kengeja.

Jana alizungumza na wananchi wa Micheweni wakati wa kukagua ujenzi wa ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya wilaya hiyo na wananchi wa Gando wilaya ya Wete wakati akizindua madarasa ya skuli ya Chekechea ya Gando.

Tangu kumalizika uchaguzi wa marudio uliofanyika mwezi Machi mwaka huu, kumekuwepo na uvumi unaoenezwa na baadhi ya viongozi wa upinzani kuwa kutafanyika mabadiliko ya uongozi kwa msaada wa mataifa ya nje.

Dk. Shein yupo kisiwani Pemba kwa ziara ya siku tano kukagua shughuli za maendeleo ambapo kesho anatarajiwa kukagua ujenzi wa barabara kadhaa zinazoendelea kujengwa katika mkoa wa Kusini Pemba.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo