Waziri wa Kenya aizulia jambo Tanzania


Suleiman Msuya

KENYA imetangaza kwamba Tanzania imejitoa katika mpango wa Viza ya pamoja wa Afrika Mashariki ikitaja moja ya sababu zake kuwa ni kuhofia ushindani na nchi hiyo.

Katika taarifa yeke iliyonukuliwa na vyombo vya habari nchini humo wiki iliyopita, Kenya kupitia Katibu wake wa Baraza la Utalii, Najib Balala ilitangaza hatua hiyo ya  Tanzania ikisema itapunguza idadi ya watalii kwa nchi za EAC.

Hata hivyo, Serikali imekanusha taarifa hizo ikieleza kwamba mchakato wa Viza ya pamoja unaratibiwa na Sekretarieti ya EAC na kwamba imesikitishwa na shutuma hizo kuelekezwa kwa Tanzania moja kwa moja.

Kaimu Mkurugenzi wa Biashara, Uwekezaji na Sekta za Uzalishaji Wizara ya Mambo ya Nje na Afrika Mashariki, Bernard Haule aliliambia JAMBO LEO mwishoni mwa wiki kwamba taarifa hizo ni za upotoshaji.

“Ni jambo la kusikitisha kuona kiongozi anatoka mbele ya vyombo vya habari anapotosha na kudanganya umma wa EAC kuwa Tanzania imegoma kujiunga katika mpango huo,” alisema Haule.

Alibainisha kuwa hakuna maridhiano yoyote yaliyokwishafanyika kuhusu mpango huo na kwamba hatua zilizofanyika ni sekretarieti kufanya utafiti wa jinsi nchi hizo zitakavyoweza kunufaika na mpango huo wa Viza moja utakapooanza.

Kaimu Mkurugenzi huyo alisema baada ya hoja hiyo kutolewa Baraza la Mawaziri la EAC liliitaka sekretarieti ya jumuia hiyo kuangalia maeneo yanayoweza kuwa na tija iwapo mpango huo utaanza kutekelezwa.

Aliyataja baadhi ya maeneo hayo kuwa ni miundombinu sahihi ya kutoa Viza ya pamoja na kila nchi mwanachama kuweza kunufaika, uwepo wa rasilimali watu wa kutosha na usalama wa Viza na nchi.

“Na sisi tumeiona taarifa hiyo kwenye mitandao na vyombo vya habari vya huko Kenya eti tumejitoa katika mpango wa Viza moja ya EAC. Ni jambo la kusikitisha kuhusishwa na suala hilo ambalo bado lipo kwenye mchakato,” alisema.

Alisema ili mpango huo uanze kufanya kazi ni jukumu la nchi wanachama kupitia EAC kukubaliana na si suala la nchi nan chi kama ambavyo inavyosemwa na Balala.

Haule aliendelea kusema zipo njama za kuichafua Tanzania katika mpango huu kwa kile alichodai kuwa nchi ya Burundi ni mwanachama ila haikutajwa kuwa imejitoa au ipo hivyo kumtaka Katibu huyo wa Baraza la Utalii Kenya kuwa muwazi ili aeleweke.

Alisema nchi ambazo zinatajwa kuingia katika hiyo Viza ya pamoja hadi sasa ni zile za Ukanda wa Kaskazini ambazo ni Kenya, Uganda na Rwanda na kwamba ili utekelezaji wake uanze ni lazima nchi zote wanachama zishiriki.

“Unajua mambo mengi ni aibu mbona Kenya imekataa kusaini mkataba wa soko la mitaji lanikini hakuna mtu ambaye anaishambulia nadhani watafute mbinu nyingine za kutoa malalamiko yo,” alisema.

Kuhusu Tanzania kutoshiriki mkutano wa masoko utakaofanyika jijini London, sababu ikiwa ni kutojiunga katika mpango huo wa Viza ya pamoja alisema si kweli na kwamba mkutano huo hauhusiani na suala hilo.

Awali, Balala alisema kama nchi tatu zilizojiunga zinataka kupiga hatua katika utalii ni vema kuboresha umoja huo na kuwa Tanzania itahyamasika kujiunga.

Alisema tatizo la nchi za Afrika Mashariki ni kuishi kwa hofu katika mambo wasiyoyajua, hali inayosababisha kila nchi kuangalia mwenzake badala ya kushindana.

Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo