Komandoo mauaji ya Vikindu alivyowatoroka Polisi


Mwandishi Wetu

IKIWA umepita mwezi mmoja na juma moja tangu polisi wapambane na majambazi kwa zaidi ya saa 6, eneo la Vikindu wilayani Mkuranga, taarifa mpya zinaeleza kwamba kiongozi wa wahalifu hao wanaodaiwa kuua polisi eneo la Mbande anayetajwa kuwa ni komando aliwatoroka polisi kupitia juu ya dari.

Taarifa hizo zimekuja siku chache baada ya watu waliokamatwa katika tukio hilo lililotokea
mkoani Pwani kuruhusiwa
kurejea kwenye nyumba hiyo ya
mapambano, huku wakihakikishiwa
ulinzi.

Habari za kiuchunguzi zinaeleza kuwa wakati polisi walipokuwa wakiendelea kutupiana risasi na majambazi hao, komandoo huyo aliyekuwa na wenzake, alitumia mwanya huo kutoboa dari, kasha bati kwa risasi na kupata upenyo wa kutoroka kupitia paa la nyumba hiyo akiwaacha polisi bila kujua alivyotoroka.

“Muda polisi wakipiga risasi kushambulia nyumba wakidhani watafanikiwa kumuangamiza, yeye alitumia muda huo kujibizana nao, huku akitoboa dari na bati kwa risasi kusaka upenyo wa kujiokoa,” kilieleza chanzo chetu.

Kiliongeza kwamba kutokomea kwa komandoo huyo kunatokana na ukweli kwamba eneo hilo la Vikindu licha ya kuwa na msitu, lina maingilio ya Bahari ya Hindi ambayo yanaweza kutumika kwa urahisi na wahalifu kutoroka.

Kwa mujibu wa mtoa habari huyo, maeneo hayo ya bahari yanamwezesha mtu kujificha na kutumia vyombo vya bahari, au miamba iliyopo baharini kutoroka, lakini pia kukimbilia kwenye visiwa vidogo vya uvuvi visivyofikiwa kirahisi na polisi.

Jambazi huyo anayetajwa kuongoza kundi la uhalifu, anaelezwa aliwahi kuwamo ndani ya jeshi na kupatiwa mafunzo ya ukomandoo katika nchi mbalimbali, ikiwamo Cuba kabla ya uraia wake kutiliwa shaka na kuondolewa jeshini. Matukio ya uhalifu anayotajwa kuhusika nayo ni pamoja na udunguaji ambapo wote waliouawa wamekuwa wakipigwa risasi za kichwa.

Siku ya tukio

Mapambano hayo ya polisi na majambazi yalitokea Vikindu Agosti 26, ambako Mkuu wa Kitengo cha Kupambana na Kuzuia Majambazi kutoka Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Thomas Njiku alipoteza maisha baada ya kupigwa risasi ya kichwa na majambazi hao wanaosadikiwa kuongozwa na komandoo huyo.

Magari ya polisi zaidi ya 16 yakifika eneo la tukio yakiwa na askari waliokuwa wameshika silaha tayari kwa mapambano. Polisi hao walivamia nyumba iliyodaiwa kuwa na majambazi hao usiku na kuanza kuifyatulia risasi kwa lengo la kuwateketeza.

Wakizungumza na JAMBO LEO jijini Dar es Salaam hivi karibuni wakazi hao walisema operesheni hiyo ilifanyika siku moja baada ya tukio la mauaji ya askari wane kwa kupigwa risasi kichwani na mtu anayetajwa kuwa ni komandoo. Kwa mujibu wa wakazi hao operesheni waliodai iliwanyanyasa, iliongozwa na Kamanda wa Upelelezi wa Wilaya ya Kipolisi Mbagala, mkoani Temeke, Thobias Walelo aliyekuwa na askari polisi pamoja na mgambo.

Wakazi hao waliozungumza na JAMBIO LEO kwa sharti la kutotajwa majina yao gazetini wakihofia usalama wa maisha yao walisema siku hiyo polisi walioongozana na mgambo waliofika eneo hilo wakiwa na magari manne na kuanza kufyatua mabomu ya machozi, hali iliyofanya washindwe kuwaona.

Mmoja wa wakazi hao alisema baadhi ya wanakijiji walikuwa wamejikusanya pamoja na walipokutwa na polisi hao na mgambo waliambiwa wakae chini na kunyosha mikono juu.

“Tuliulizwa kwa nini ninyi mmejenga maeneo yasiyoruhusiwa, nilikamatwa nikiwa pembeni kidogo na nyumba yangu na wakati wanaingia na kurusha mabomu ilikuwa ni saa 11 jioni na kashikashi hizo zilidumu hadi saa moja usiku,” alisema.

Kamanda wa upelelezi wa Wilaya ya Kipolisi Mbagala, Thobias Walelo alisema hawezi kuzungumzia tukio hilo kwa kuwa hana mamlaka.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi huo, Gilles Muloto alisema hana taarifa za tukio hilo na kwamba ni mara yake ya kwanza kulisikia hivyo hawezi kulizungumzia na kulitaka gazeti hili lifuatilie tena taarifa hizo kwa kuwa eneo hilo halimhusu.

Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo