Lipumba atumie busara—Wasomi


Fidelis Butahe

SIKU moja baada ya Mwenyekiti wa CUF anayetambuliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Profesa Ibrahim Lipumba kuwasimamisha kazi wakurugenzi sita wa idara za chama hicho, wasomi wamemtaka kutumia busara ili kunusuru mvutano na vurugu zinazoweza kukikumba chama hicho.

Wamesema licha ya kuwa mtaalamu huyo wa uchumi kuwa anasimamia Katiba ya chama hicho kurejea katika nafasi yake, lakini ni jambo la kushangaza kutaka kurejea katika wadhifa huo takribani mwaka mmoja baada ya kujiuzulu, huku wakihoji alisahau nini.

Juzi Lipumba alitangaza kuwasimamisha kazi wakurugenzi hao kutokana na changamoto zinazokikabili chama hicho, jambo lililopingwa na Kaimu Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Mawasiliano ya Umma wa CUF, Ismail Jussa Ladhu aliyeeleza kwamba Lipumba hana uwezo huo na kusisitiza wakurugenzi hao wanaendelea na majukumu yao kama kawaida.

Katika maelezo yake, Profesa Lipumba alisema atateua watakaokaimu nafasi hizo hadi watakapothibitishwa na Baraza Kuu la Uongozi la Taifa.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Ruaha, Profesa Gaudence alisema: “Lipumba atumie busara tu. Hivi hii hali iliyopo CUF anaionaje? Alijiuzulu mwenyewe sasa anarudi vipi? Alipaswa ajipime mwenyewe; je, anakubalika? Maana mkutano mkuu wajumbe zaidi ya 400 walipinga kurejea kwake katika uongozi.”

“Kwa kilichotokea katika mkutano huo alipaswa tu kukaa kando. Hata vyama vinavyounda Ukawa havipo pamoja naye sijui atafanyaje kazi. Atasimamia wapi,” alisema msomi huyo Wakili na mhadhiri wa Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM), Dk James Jesse alisema:

“Kujiuzulu na kukaa mwaka mzima kasha kutangaza kurejea ni jambo ambalo halikubali kisheria na kikatiba.” Alisema kwa uamuzi huo wa kujiuzulu, kuendelea kumtambua Profesa Lipumba kama mwenyekiti wa CUF licha ya kuwa anatumia Katiba ya chama hicho kueleza uhalali wake si sahihi.

Hata hivyo, akizungumzia uamuzi wake, Lipumba alisema: “Katiba inasema (mwenyekiti) anashauriana na makamu mwenyekiti katika kuteua, ila katika kubadilisha mimi ndio nabadilisha na kupeleka majina katika Baraza Kuu la Uongozi Taifa kuthibitisha.”

Alipoulizwa kama hilo litawezekana kutokana na baraza hilo kupiga kura ya kumvua uanachama alisema: “Ni mpaka wakati ukifika…, nitapeleka majina katika Baraza Kuu ili kuthibitishwa. Kuna kazi ngumu, ila nina nia ya umoja na kufanya kazi ya pamoja kwa ajili ya kujenga chama pande zote mbili za muungano.”
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo