Mwinyi asema Taifa limepoteza mwelekeo


* Hakuna mwenye maono ya Nyerere, wala wa kufuatwa
*
Asikitishwa na ‘panya road’ asema ni mfano wa maadili


Suleiman Msuya

“TAIFA limepoteza mwelekeo. Balaa ambalo tumepata miaka 17 ya kutokuwepo Mwalimu Nyerere tunapaswa kufakari ili turejeshe taifa kwenye reli yake,"

Hivyo ndivyo alivyosema Rais mstaafu wa Awamu ya Pili, Alhaji Ali Hassan Mwinyi jana katika Kongamano la Kumbukumbu ya miaka 17 ya Kifo cha Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere lililofanyika jijini Dar es Salaam.

Nyerere alifariki dunia Oktoba 14, 1999 katika Hospitali ya Mtakatifu Thomas, Uingereza alipokuwa akitibiwa saratani ya damu na kuzikwa kijijini kwake Butiama mkoani Mara.

Katika kongamano hilo lililoandaliwa na Taasisi ya Uongozi, Mwinyi alisema Taifa linapaswa kujadili ni wapi watu wake wamekosea na sababu yake ili kuweza kumuenzi Nyerere.

“Tangu Nyerere alipofariki dunia, Taifa limekuwa na mmomonyoko wa maadili, huku ikionekana dhahiri kuwa hakuna wa Mtanzania mwingine wa kufuatwa,” alisema Mwinyi.

Rais mstaafu huyo alisema ni jambo la kusikitisha kuona kunakuwapo kundi linaloitwa 'Panya roads' huku kukiwa hakuna hatua za kueleza sababu na kukukabiliana nalo.

"Nadiriki kusema Taifa limepoteza mwelekeo na mbaya zaidi kuna kila dalili kuwa hakuna mwenye maono ya Nyerere kurejesha maisha yake kwa jamii yetu," alisema Mwinyi maarufu kama Mzee Ruksa.

Alisema kwamba hayati Baba wa Taifa alikuwa zaidi ya kiongozi, hali ambayo ilimwezesha yeye (Mwinyi) kufikia alipofikia lakini kwa siku za karibu kumekuwa na uvunjifu wa maadili katika uongozi.

Mwinyi alisema ni jukumu la kurejea katika mafundisho ya Mwalimu ili kuweza kurejesha heshima ya nchi ambayo kwa sasa imekosa wakuigwa.

Alisema malalamiko ambayo yanaendelea katika jamii leo ni ishara tosha kuwa tunapaswa kujitafakari kama Taifa linalotaka kumuenzi Nyerere.

Mwinyi alisema kinachoonekana ni kama gari limekatika usukani hivyo makongamano ya Kumbukumbu ya Nyerere litumike kutafakari hatma ya Taifa.


Alisema Nyerere aliondoka akaacha nchi ikiwa maskini na hadi sasa haijawa tajiri ila wapo matajiri wachache ambao wanaendelea kuleta mpasuko.

Alisema Nyerere  aliamini katika ukweli, uadilifu ambao  ulichangia ukombozi na kujiamini ila leo imefikia kuzalisha hadi panya roads ambao zamani  hawakuwepo.

Rais Mwinyi alisema katika ulimwengu wa sasa askari wanaogopwa na kukimbiwa hivyo ni jukumu la jamii kujiiza nini sababu.

Aidha, Mwinyi alihoji nini sababu ya udini kushika kasi kwa siku za karibuni na kwamba utaratibu huo haupaswi kuwa msingi wa maisha ya Mtanzania .

Rais mstaafu Mwinyi alisema leo imefikia watu wanaogopa kutaja majina ya ukoo wakihofia kukosa kazi jambo ambalo halikuwepo kwa utawala wa Nyerere.

"Tusikubali kuliacha taifa kama kishada kilichokatika uzi, inakuwaje nchi inakuwa    kama haina mwenyewe, hakuna mwenye sauti Mwalimu hakutuacha hivi, " alisema.

Kwa upande wake Profesa Issa Shivji alisema katika kumuenzi Mwalimu watanzania wanapaswa kuangalia mambo matatu ambayo ni falsafa yake, msingi wa umoja wa kitaifa na azimio la uongozi.

Alisema kupitia misingi hiyo Nyerere aliweza kuishi na makundi yote bila tatizo jambo ambalo kwa sasa halipo.

"Uongozi ni njia ambayo inahitaji ushikiano na si kufikiria utawala huwezi kufika hasa katika kizazi hiki cha kuhoji, " alisema.

Mkurugenzi mstaafu wa Idara ya Usalama wa Taifa (TISS), Dk. Hans Kitine alisema katika miaka 17 ya kutokuwepo kwa Nyerere Taifa limegubikwa na rushwa ya hali ya juu hali inayosikitisha.
Kitine alitoa rai kwa washauri wa Rais John Magufuli kumshauri kuhusu uongozi pamoja na kutambua kuwa Rais ni taasisi na si mtu mmoja.

“Mimi siogopi kusema hili pamoja na kuwa halikuwa katika ajenda naomba washauri wa Rais wamshauri kuwa Rais ni taasisi si mtu binafsi na nikipata nafasi nitaenda kumueleza,” alisema Kitine.

Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe aliyehudhuria kongamano hilo alisema: “Jitihada alizofanya Mwalimu katika kujenga demokrasia zilisimamia hoja, lakini kwa sasa ukiwa na hoja unapata misukosuko. Mfano leo hii, Rais amezuia watu kwenda kwenye sherehe za kuzima Mwenge, Hivi ameshirikisha nani wakati fedha hizo zilipitishwa bungeni?”

Msaidizi wa mwisho wa Nyerere, Samweli Kasoli alisema ujumbe alioachiwa na Baba wa Taifa ni Watanzania kutomlilia yeye bali walilie Tanzania yao.


Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo