Waathirika wa tetemeko wachangiwa milioni 660/-


Mwandishi Wetu

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amepokea michango yenye thamani ya Sh milioni 660.25 taslimu, hundi na vifaa kwa ajili ya wananchi walioathirika na tetemeko la ardhi mkoani Kagera.

Makabidhiano ya michango hiyo, yalifanyika juzi ofisini kwake Dar es Salaam.

Akikabidhi hundi kwa Waziri Mkuu, Makamu wa Rais wa Kampuni ya ACACIA, Deodatus Mwanyika alisema walitoa Sh milioni 325 na tayari zilishaingia kwenye akaunti ya maafa.

Aliomba wadau wengine na taasisi nchini wajitokeze kuisaidia Serikali kukabiliana na janga hilo kwani mahitaji halisi ni makubwa kuliko kiasi kilichokusanywa hadi sasa.

Wadau wengine waliochangia ni Balozi wa Japan nchini, Masaharu Yoshida na Shirika la Misaada la Maendeleo la Japan (JICA), ambao walitoa vifaa vyenye thamani ya Sh milioni 220.

Vifaa hivyo ni mahema 220, mablanketi 1,100; vigodoro vyepesi 1,110; madumu ya maji 250 na mashuka ya plastiki 22. 

Mkurugenzi Mkuu wa TBC1, Dk Ayoub Rioba alikabidhi hundi za Sh milioni 41.55, akisema kama taasisi waliguswa na  maafa ya Kagera wakatafuta njia ya kuchangisha ili kuisaidia Serikali kukabiliana na tatizo hilo.

“Tuliamua kufanya harambee na kuhamasisha wananchi wachangie ambapo wengine walileta kwetu na wengine wakapeleka moja kwa moja Kagera. Na leo tunakabidhi kiasi ambacho tulikusanya kupitia harambee hiyo,” alisema.

Wengine waliokabidhi michango yao, ni Makamu Mwenyekiti wa Umoja wa Wenye Magereji Tegeta, Leonard Mwanjela ambaye alitoa Sh. milioni mbili kwa niaba ya mafundi gereji wa wilaya ya Kinondoni.

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Kariakoo (JWK), Abdalla Mwinyi alisema walifanya harambee na kupata Sh milioni 60.8 ambazo walinunulia nguo, magodoro na unga wa mahindi tani 10.

Taasisi ya Wakaguzi wa Ndani ilikabidhi Sh milioni 6.7. Mwenyekiti wa Bodi wa Taasisi hiyo, Richard Magongo alisema baada ya kuona hilo, walichangishana na kupata kiasi hicho cha fedha.

Mkurugenzi wa Kampuni ya Sura Technologies,  Ramadhar Reddy alikabidhi hundi ya Sh milioni 5.  

Akitoa shukrani kwa waliotoa michango hiyo, Waziri Mkuu aliahidi Serikali kuhakikisha michango hiyo inafikishwa Kagera kwa walengwa.

“Tunawashukuru sana kwa michango yote. Kutoa ni moyo na si utajiri. Naomba Watanzania wengine mwendelee kujitokeza ili kusaidia wenzetu waliokumbwa na maafa haya,” alisema.

Pia alishukuru wanahabari kwa kuwapa wananchi taarifa za matukio hayo na kuhamasisha wachangie ndugu zao waliokumbwa na maafa.  Tetemeko hilo lilitokea, Septemba 10 na kusababisha vifo vya watu 17 na wengine 440 kujeruhiwa.

Pia lilibomoa nyumba 2,063 huku zingine 14,081 zikiwa katika hali hatarishi baada ya kupata nyufa na 9,471  uharibifu mdogo huku wananchi 126,315 wakihitaji misaada.


Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo