Mambo yaliyotikisa utawala wa JPM



MWAKA MMOJA MADARAKANI

Fidelis Butahe

SIKU 20 kabla ya Rais John Magufuli kukamilisha mwaka mmoja madarakani Novemba tano mwaka huu, kuna mambo manane ambayo yanaweza kutajwa kuwa ndiyo yaliyotikisa taifa katika utawala wake.

Mambo hayo kati ya mengi, yamelitetemesha Taifa kwa nyakati tofauti kutokana na kasi ya Rais Magufuli kiutendaji, huku baadhi ya watu wakifurahia hatua hizo na wengine kuumia na kunung’unika kwa kuguswa katika maeneo yao ya utendaji.

Baadhi ya mambo hayo ni kufuta safari za nje, kufuta sherehe za kitaifa, kutangaza Serikali kuhamia Dodoma na kuondoa watumishi hewa

Mambo mengine ni kuzuia mikutano ya siasa, ‘kutumbua’ watendaji wa Serikali na taasisi zake, kuzuia taasisi zake na zile za umma kutumia kumbi za mahoteli au za kukodi kwa kufanya makongamano na mikutano.

Jambo jingine ni lile la wiki iliyopita alipowataka  watendaji wote wa Serikali walioalikwa katika sherehe za Kilele cha Mbio za Mwenge kutohudhuria hafla hiyo na kurejesha posho walizopewa.

Waliozuiwa kuhudhuria sherehe hizo ni pamoja na wakuu wa mikoa, wilaya, wakurugenzi wa halmashauri, makatibu tawala na wakuu wa idara mbalimbali.

Wasomi na wachambuzi wa masuala ya siasa wametaja baadhi ya mambo hayo kuwa yamekuwa na tija kwa taifa, lakini wakaponda mengine wakisema hayakuwa na msingi kufanywa.

Walichosema

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Richard Mbunda alisema mambo hayo ni mazuri na kwa sababu rais ana madaraka makubwa, akiyatumia vyema anaweza kuliletea Taifa maendeleo.

“Sidhani kama marais waliotangulia na hata baadhi ya watu walitarajia kuona haya anayofanya Magufuli.  Watanzania sasa wanatakiwa kutazama uwezo wa kiongozi kuliko kuvutiwa na chama,” alisema Mbunda.

Alisema Tanzania ni nchi masikini hasa katika miundombinu na huduma za jamii, lakini umasikini huo unaweza kuondoka iwapo nchi itapata viongozi wenye kufikiria maendeleo. Alitolea  mfano uthubutu wa Rais kulifufua Shirika la Ndege Tanzania (ATCL).

Mhadhiri wa Chuo Kikuu Huria (OUT) Hamad Salim, aliungana na Mbunda katika hoja ya kutaka nchi kuwa na maendeleo, lakini akasisitiza kuwa ni lazima iwe na mwongozo utakaofuatwa na viongozi wote.

“Rais anafanya mambo mazuri lakini binafsi naona kuna tatizo. Mwalimu Nyerere (Julius-Rais wa Awamu ya Kwanza), alianzisha Azimio la Arusha akitaka nchi iongozwe chini ya mwongozo wa azimio hilo. Rais wetu (Magufuli), hana mwongozo wowote ndio maana kuna maamuzi yanatolewa tolewa tu. Watendaji hawajui nini wanapaswa kufanya na kwa wakati gani,” alisema Salim.

Aliongeza: “Nchi yetu ilipopata Uhuru, Nyerere aliona wazi kuna vitu vinakosekana kwa kuwa kila mtu alifanya mambo ajuavyo. Ndio maana akaja na Azimio la Arusha. Magufuli amekuwa akizungumza mambo mengi ila hajatueleza nini kinatuongoza na kuna mambo yanatokea kwa sababu hatuna mwongozo.”

Akitolea mfano jinsi watendaji wanavyobanwa na kurejesha fedha licha ya kuwa zimeshaidhinishwa kwa shughuli mbalimbali alisema: “Wizara ya Fedha inazipeleka hizo fedha kwa wahusika kwa sababu wahusika wanafuata mwongozo na taratibu za Serikali iliyopita. Magufuli aje na mwongozo wake ijulikane msimamo na mtazamo wa Serikali yake.”

Alisema wapo baadhi ya watendaji wa Serikali wanaoshindwa kutoa uamuzi kwa kukosa mwongozo na baadhi kuogopa kuamua jambo kwa kuhofia kutumbuliwa na mamlaka zao za uteuzi.

Watumishi hewa

Mara baada ya kuingia madarakani, Rais Magufuli alitangaza kiama kwa watumishi hewa na katika maadhimisho ya Sikukuu ya Wafanyakazi (Mei-mosi), alibainisha kuwapo kwa watumishi hewa 10,295 serikalini, kati  yao watumishi hao, 8,373 wanatokea Tamisemi na 1,922 wanatoka Serikali Kuu.
Hivi karibuni katika uzinduzi wa ndege mpya za ATCL, alitaja tena takwimu hizo.

Kufuta sherehe

Novemba 8 mwaka jana, siku tatu baada ya kuapishwa kuiongoza Tanzania, Rais Magufuli alitangaza kuokoa Sh225 milioni zilizochangwa kugharamia hafla ya wabunge na kuagiza zinunulie vitanda kwa ajili ya Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).

Pia, alifuta Sherehe za Uhuru Desemba 9, mwaka jana na kuamuru Sh bilioni 4 zilizokuwa zimetengwa zitumike kupanua Barabara ya Morocco-Mwenge.

Pia aliahirisha sherehe za Muungano, Aprili 26 na kuokoa Sh bilioni 2 na kutaka zitumike katika upanuzi wa Barabara ya Ghana hadi Uwanja wa Ndege wa Mwanza.

Kufuta safari za nje

Novemba 7, mwaka jana, Rais Magufuli alitangaza kufuta safari za nje ya nchi hadi hapo maamuzi mengine yatakapotolewa.

Alisema shughuli zote zinazotakiwa kufanywa nje ya nchi zifanywe na kusimamiwa na mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania nchi za nje na wale watakaosafiri ni kwa vibali maalum.

Kuhamia Dodoma

Muda mfupi baada ya kukabidhiwa kijiti cha uenyekiti wa CCM, Rais Magufuli alitoa kauli ya kutaka Serikali kuhamia Dodoma, huku akisisitiza atahakikisha Serikali yote inahamia mkoani humo kufikia mwaka 2020.

Kusitisha mikutano ya siasa
Juni 23 mwaka huu, Rais Magufuli alipiga marufuku vyama vya siasa kufanya ushindani wa siasa hadi baada ya miaka mitano ili wananchi wahoji wanasiasa kama wametekeleza yale waliyoyaahidi katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.

Mikutano ya taasisi za Serikali
Katika hotuba yake bungeni Novemba 20, 2015, Rais alitangaza hatua kadhaa za kubana matumizi, zikiwemo za warsha, semina, makongamano na matamasha kufanyika katika kumbi za taasisi za Serikali au wizara jambo ambalo kwa kiasi fulani lilisababisha hoteli kupoteza wateja wake wa uhakika, ambao ni taasisi za Serikali.

Kutumbua majipu

Mara baada ya kuapishwa, aliahidi kuwashughulikia watendaji wazembe ili Serikali yake iondokane na kuwalipa watu mishahara bila kufanya kazi yoyote.

Uamuzi wake huo umesababisha zaidi ya watumishi 100 kutumbuliwa kutokana na tuhuma mbalimbali, huku baadhi yao wakifikishwa mahakamani kwa tuhuma mbalimbali.


Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo