Lipumba akataliwa baada ya ziara


Sijawa Omary, Lindi

SIKU chache baada ya Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba kufanya ziara ya mafanikio Kusini mwa nchi, CUF mikoa ya Kusini ya Lindi na Mtwara imetoa tamko la kutomtambua kuwa Mwenyekiti wake halali.

Tamko hilo lilitolewa hivi karibuni na wajumbe wa Baraza Kuu la Uongozi huo Taifa  na baadhi ya wadhamini wa chama hicho wakati wa mazungumzo na vyombo vya habari mikoani humo  baada ya kumalizika kwa kikao cha Kamati ya Utendaji ya Kanda kwenye ofisi za chama hicho mjini hapa.

Aidha,  kikao hicho kilishirikisha wajumbe mbalimbali akiwamo mdhamini wa CUF, Abdallah Khatau kutoka Masasi,  Mbunge wa Tandahimba, Ahmadi Khatani, Mbunge wa Kilwa Kusini Selemani Bungara ‘Bwege’, Mwenyekiti wa CUF wa Wilaya ya Lindi Mjini, Salum  Bar’wani na viongozi wengine.

Bar’wani wakati akiwasilisha tamko hilo kwa niaba ya wajumbe wenzake,  alitaja sababu zilizofanya wafikie uamuzi huo kiwa ni   kitendo cha kujiondoa kwenye nafasi yake wakiwa kwenye mapambano ya uchaguzi.  

Pia alitaja sababu zingine kuwa ni kutekeleza na kuheshimu uamuzi halali wa uongozi wa Baraza Kuu la CUF lililokutana   Zanzibar.

Alisema kitendo cha Lipumba kuwaacha kwenye mazingira magumu ya uchaguzi  huku wanachama na wazee wakimsihi kuacha lakini kuendelea na msimamo wake ni cha kushangaza hivyo hawako tayari kufanya kazi naye kutokana na udhaifu alioonesha awali.

Kutokana na hilo, wajumbe hao walikanusha tamko la baadhi ya watu wanaojiita viongozi na kwamba wanamuunga mkono Profesa.

‘’Baadhi ya watu wamekuwa wakitoa maneno ya uongo kwa chama cha CUF, sisi viongozi tunapenda kukanusha maneno haya na hatukubaliani nayo,’’ alisisitiza Bar’wani.

Alisema,  wanaungana na viongozi wenzao kupinga alichokiita msimamo wa ushauri wa Msajili wa Vyama vya Siasa Nchini, Jaji Francis Mutungi kwamba ushauri wa kumrejesha na kumtambua Lipumba kuwa kiongozi ni kinyume na Katiba ya CUF.

Tamko hilo liliwataka watendaji wa wilaya wa kanda hiyo kutomuunga mkono Lipumba kwa kuwa si kiongozi anayeitakia mema CUF huku wakiomba wanachama kuwa na subira wakati viongozi wa kitaifa wakiendelea kushughulikia mgogoro huo.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo