Matumaini ya walalahoi ‘kuonja’ ndege yatoweka


Fidelis Butahe

SAA chache baada ya Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) kuanika nauli za ndege mpya za Bombardier Dash 8 Q400 zilizonunuliwa hivi karibuni na Serikali, viongozi wa vyama vya NCCR-Mageuzi na CUF wamesema haziendani na kauli ya Rais John Magufuli aliyeahidi kuwa nauli itakuwa chini.

Wamesema nauli hizo zinaonesha wazi kuwa Serikali inalenga zaidi kufanya biashara kuliko huduma stahiki na kudai kuwa zinatofautiana kwa kiasi kikubwa na nauli za ndege za mashirika mengine.

Wakati Mwenyekiti wa NCCR, James Mbatia akiitaka Serikali kupitia upya nauli hizo kwa madai kuwa ndege hizo zimenunuliwa kwa kodi za wananchi, Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya CUF, Julius Mtatiro alisema lazima nauli hizo ziendane na ubora wa huduma.

Kwa mujibu wa taarifa katika tovuti ya Shirika hilo,  nauli hizo zimegawanywa katika makundi mawili ya daraja la kwanza na la pili, huku nauli ya juu kwa daraja la kwanza ikiwa ni Sh 590,000 kutoka Dar es Salaam kwenda Kigoma, na iwapo abiria atakata tiketi ya kwenda na kurudi atalazimika kulipa Sh 910,000.

Katika daraja la pili, usafiri wa juu wa ndege hizo pia ni kutoka  Dar es Salaam kwenda Kigoma ambao ni Sh 395,000 na kufuatiwa na Dar es Salaam kwenda Tabora, Sh 385,000.

Katika mpangilio wa safari 14 za ndege hizo katika mikoa nchini, nauli ya chini kabisa ni kutoka Dar es Salaam hadi Zanzibar   ni  Sh 85,000 huku kutoka Dar es Salaam kwenda mikoa ya  Arusha, Mtwara, Dodoma, Tabora, Mbeya, Kilimanjaro na Bukoba mkoani Kagera, nauli ni kati ya Sh180,000 na Sh 520,000 kwa madaraja yote,  mbali na kukata tiketi ya kwenda na kurudi.

Kwa mujibu wa maelezo ya watoa huduma wa Shirika hilo, nauli hizo zitatumika kwa siku 14, kuanzia kesho hadi Oktoba 28 na baada ya hapo zitaongezwa kulingana na eneo husika ambalo ndege hizo zitakwenda.

Septemba 28 wakati akizindua ndege hizo, Rais Magufuli alisema nauli hazitakuwa kubwa na kila Mtanzania ‘ataonja’ ndege, kubainisha kuwa zinatumia mafuta kidogo na zinatua katika viwanja vya mazingira yote nchini.

“Nauli za ndege hizi ziko juu kuliko za Fastjet. Watanzania wanahitaji usafiri wa uhakika na kama Serikali ikiweza kulisimamia hilo huenda watu wakasahau machungu ya nauli za juu…ila nikiri wazi nauli hizi ni kubwa kwa kweli, inasikitisha sababu zitaongezeka badala ya kupungua,” alisema Mtatiro.

Mbatia alisema: “Wanapaswa kutazama mashirika mengine duniani yanafanyaje. Hii ni biashara ya ushindani. Ninachokiona ni Serikali kujikita katika biashara bila kuangalia hali halisi.

“Kabla ya kuja na nauli hizi lazima ujiulize, je huduma zimezoeleka na watu? Na je, wataweza kutoa ushindani kwa wengine?”

Alisema kiwango hicho cha nauli kinaonesha kuwa ATCL imeanza kwa kushindwa na imeshindwa kuanza kazi kwa kuzingatia misingi ya uzalishaji na ufanisi.

“Wangeweza kufanya ushindani kwa kuanzisha safari za ndege katika nchi kama za Kongo, Zimbabwe na Nigeria, ambako watu hulazimika kuunganisha ndege kuliko kuanza kupambana hapa nyumbani,” alisema.

Alibainisha kuwa tatizo analoliona ni siasa kuingizwa katika biashara na kushauri wanasiasa kuacha watalaamu wa masuala ya anga kufanya kazi yao.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo