LHRC: Wahaini, magaidi, wauaji wasinyongwe


Dotto Mwaibale

KITUO cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), kimefungua kesi ya kikatiba kuhusu ulinzi wa haki ya kuishi na urekebishwaji wa sheria ya kanuni ya adhabu juu ya ulazima wa kutolewa adhabu ya kifo kwa makosa ya uhaini na mauaji.

Kesi hiyo imefunguliwa dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali  kikitaka ufafanuzi zaidi juu ya adhabu ya kifo, kikibainisha kuwa adhabu hiyo haimpi nafasi mtuhumiwa kujirekebisha bali ni kulipiza kisasi.

Kituo hicho kimesema endapo Tanzania itatekeleza hukumu ya kifo  kwa sasa, inamaanisha watu wapatao 228 na zaidi watapoteza maisha yao huku wengine 244 wakisubiri rufaa zao.

Akizungumza juzi Dar es Salaam, wakati akitoa tamko la kupinga adhabu ya kifo, Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Hellen Kijo-Bisimba alisema hadi  mwaka jana jumla ya watu 472 walikuwa wamehukumiwa kunyongwa.

Alisema Kituo kinaiomba Serikali kurekebisha sheria ya kanuni ya adhabu na sheria ya ugaidi yenye kutoa adhabu ya kifo kwa makosa ya mauaji, uhaini na ugaidi.

Dk Kijo-Bisimba alisema Kituo kina sababu za kupinga adhabu ya kifo na  hakifurahii watu kuua wengine na ndiyo maana hakipendi pia muuaji auawe.

“Adhabu ya kifo ni vigumu kuhakikisha kuwa inatekelezwa tu kwa ambao huwezi kuirekebisha, kwani mfumo wa utoaji haki huwa pia na mianya ya makosa na hivyo maisha ya mtu yanaweza kupotea bure,” alisema Dk Kijo-Bisimba na kuongeza kuwa hakuna ushahidi   kuwa adhabu hiyo inaweza kuzuia wengine kutenda makosa kama hayo.

Alisema licha ya adhabu  hiyo kutotekelezwa nchini kwa takriban miaka 22 sasa, taarifa zinaonesha kuwa watu 72 walishanyongwa.

Hata hivyo, aliiomba Serikali kutengeneza utaratibu wa kuelimisha jamii juu ya kuheshimu haki za binadamu hususan za kuishi na kuweka mazingira ya kuiheshimu haki hiyo.

Pia aliomba ibadilishe sheria kwa kuondoa adhabu ya kifo na kuweka mbadala kwenye makosa ya jinai na kwa wafungwa waliopo mfano vifungo vya muda mrefu  gerezani.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo