Bakhresa kuongeza viwanda nchini

Abraham Ntambara

MKURUGENZI Mtendaji wa Kampuni ya Bakhresa Foods, Said Salim Bakhresa, amesema ataongeza viwanda vingine vya usindikaji matunda nchini ili kuongeza thamani kwa mazao ya wakulima.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotumwa na Ofisi ya Waziri Mkuu jana Dar es Salaam kwa vyombo vya habari, ilisema kauli hiyo ilitolewa na Mkurugenzi huyo  alipokutana na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na kufanya naye mazungumzo ofisini mwake.

Bakhresa alisema ana mpango wa kujenga kiwanda katika mikoa ya Kanda ya Ziwa na  amefikia uamuzi huo baada ya kubaini kuwa watu wanapata usumbufu wa kusafirisha matunda hadi Dar es Salaam kuyauza.

“Kuanzia Oktoba 15, tutaanza kupokea matunda kutoka Kahama na maeneo ya jirani, na kwa siku tunapata malori zaidi ya 30 na yakimalizika tunaanza kupokea ya  mikoa ya Pwani na Kusini,” ilisema taarifa ikimkariri Bakhresa.

“Tukijenga kiwanda Kanda ya Ziwa, tutapunguza adha ya wadau kusafirisha matunda kutoka kule hadi hapa kiwandani na badala yake sisi tutakuwa tunasafirisha juisi isiyochujwa na kuileta hapa kwa hatua zaidi za usindikaji,” alisema.

Aliongeza kuwa ana mpango wa kuendeleza usindikaji wa vyakula vya nafaka kwenye mikoa ya Kusini na kwamba hadi sasa ameajiri wafanyakazi zaidi ya 8,000 wakiwamo Watanzania 180 kwenye matawi yake nje ya nchi ambapo hulipwa kama wataalamu.

Alisema hivi sasa Kampuni hiyo imeshafungua matawi mengine Rwanda, Burundi, Msumbiji, Malawi, Zimbabwe na Afrika Kusini.

Kampuni ya Bakhresa Foods inatengeneza juisi, soda, maji, biskuti, barafu, ngano, mahindi, mchele na bidhaa za kuokwa.

Waziri Mkuu Majaliwa alimweleza  Bakhresa kuwa nia ya Serikali ni kushirikiana na wafanyabiashara na wamiliki wa viwanda kwa kuwa imedhamiria kukuza uchumi kupitia uzalishaji viwandani.

“Serikali inathamini mchango wa wenye viwanda katika nchi yetu, tunawashukuru ninyi ambao ni wakongwe kwenye sekta hii, na kwa hiyo tunawaomba msikate tamaa, endeleeni kufungua viwanda zaidi ili wananchi wapate mahali pa kuuzia mazao au bidhaa zao,” alisema.

Alimwomba Bakhresa aangalie maeneo mengine zaidi ya kuwekeza kama vile kwenye sekta za hoteli na utalii ili kusaidiana na Serikali kukuza uchumi wa Tanzania.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo