JPM aasa watoto wa Masaburi washikamane


Sharifa Marira na Hussein Ndubikile

RAIS John Magufuli ameasa watoto wa marehamu Didas Masaburi kushikamana.

Alitoa wosia huo jana wakati wa kuaga mwili wa marehemu Meya huyo wa zamani wa Jiji la Dar es Salaam kqwenye viwanja vya Karimjee na baadaye kuzikwa jana Chanika.

Rais Magufuli alisema unapotokea msiba shetani hupata nafasi ya kujipenyeza kwenye familia na kuwahimiza kuwa wamoja kwa kuwa baba yao aliwapenda na ndiyo maana hakuwabagua.

‘’Naomba mshikamane, mtoto mkubwa wa marehemu awe kiongozi wa familia, nafahamu uchungu mlionao msiruhusu shetani aingie ndani ya familia,” alisema Magufuli.

Awali Rais alisema baadhi ya Waafrika kuwa na wake watano hadi 10 ni kawaida.  

Alitoa kauli hiyo kwa nia iliyoonekana ya kujaribu kuzima minong’ono na sintofahamu iliyoibuka baada ya wasifu wa marehemu kueleza kuwa ameacha mke mmoja, wajane na watoto 20.

‘’Tumetambulishwa hapa mke mmoja, lakini mimi nafahamu wako wanne au watano hivi. Tabia zetu za kiafrika kuwa na wake wanne, watano, sita au 10 ni kawaida hata Mfalme Suleiman  alikuwa na wake 1,000. Tunamsoma kwenye vitabu (vya dini) hivyo naombeni mshikamane,” alisema Rais Magufuli.

Baada ya kauli hiyo muda mfupi  kabla ya kuanza ratiba ya kuaga mwili, Rais alishangiliwa kwa kupigiwa makofi na vigelegele na baadhi ya ndugu wa marehemu.

Rais alilazimika kueleza hayo baada ya awali msemaji wa familia, Machabe Masaburi kwenye wasifu wa marehemu kueleza kuwa ameacha mke wa ndoa na wajane, bila kutaja idadi yao, jambo lililozua minong’ono miongoni mwa ndugu na jamaa ambao tangu awali walionekana kukaa kwa makundi.

Rais Magufuli ambaye wakati wasifu wa marehemu ukisomwa alikuwa akiteta jambo na mtangulizi wake, Jakaya Kikwete alisema: “Najua hata watoto wako zaidi ya 20…, nilikuwa nateta na Kikwete, tulitamani hata sisi tungekuwa na wake wa namna hiyo.”

Maelezo ya Machabe yalionekana wazi kuchanganya ndugu huku baadhi wakisikika wakisema maelezo yake hayakuwa sahihi, lakini hali ilibadilika baada ya Rais kumaliza kuzungumza.

“Amefanya kitu cha msingi sana kwa kweli, maana hali haikuwa nzuri hapa,” alisikika akisema mmoja wa ndugu wa marehemu ambaye hakuwa tayari kutajwa jina lake gazetini.

Mwingine aliiambia JAMBO LEO, kuwa Meya huyo wa zamani   alikuwa na wake watano na mmoja aliyejulikana kwa jina la Nyangeta alifariki dunia, na kubaki wanne ambao ni Janeth, Zulpa, Grace na Anna.

Masaburi ambaye alikuwa Meya wa Jiji la Dar es Salaam kati ya mwaka 2010 na mwaka jana na kugombea ubunge wa Ubungo mwaka jana alifariki dunia Jumatano iliyopita.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo