CWT yalia na madai ya walimu


Abraham Ntambara

Gratian Mukoba
CHAMA cha Walimu Tanzania (CWT) kimeeleza kutoridhishwa na kasi ya Serikali katika ulipaji wa madeni yao, ikilinganishwa na kiasi cha fedha wanachodai.

Rais wa CWT Gratian Mukoba, amesema hayo jana alipozungumza na mwandishi wa gazeti hili jijini Dar es Salaam jana, ambapo alisema kasi ya ulipajia wa madeni hayo ni ndogo.

Alifafanua kama angekuwa mshauri wa Rais John Magufuli, angemshauri kufumba macho kwenye makusanyo ya mwezi huu na kuchukua kiasi cha Sh bilioni 350 na kuwalipa walimu, kama alivyofumba macho na kuchukua Sh bilioni 750 za kununulia ndege tatu.

“Serikali inahitaji Sh bilioni 350 ili kulipa madeni yote ya walimu, lakini kasi inayotumiwa na Serikali kulipa deni hili ni ndogo ukilinganisha na kiasi walimu wanachodai,” alisema Mukoba.

Alisema Serikali inatakiwa kulipa madeni hayo, ili walimu wafurahie na kuona wanaongozwa vyema na Serikali ambayo Rais, Waziri Mkuu na wake zao ni walimu.

“Ushauri wangu mimi kwa Serikali ni kama vile Rais Magufuli alivyofumba macho akachukua Sh. bilioni 750 akanunua ngege tatu akazileta, afanye hivyo hivyo kwa makusanyo ya mwezi huu, achukue Sh. bilioni 350 alipe deni la walimu,” alisema Mukoba.

Alisema katika Jiji la Dar es Salaam peke yake, walimu wanadai Sh. bilioni tatu; Mbeya na Mbozi madai ni takribani Sh. milioni 400 huku Ileje walimu wakidai Sh. milioni 300 huku madeni hayo na majina ya walimu yakiwa tayari Ofisi ya Rais tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi).

Mukoba alisema hata madai ya walimu waliostaafu hawajalipwa kutoka katika Mfuko wa Pensheni kwa Watumishi wa Umma (PSPF), kwa kuwa Serikali bado haijawasilisha fedha hizo katika mfuko huo.

Alisema kiasi cha fedha wanachodai walimu hao wastaafu ni takribani Sh. bilioni 150, ambazo Serikali inatakiwa kuwasilisha kiasi cha Sh. bilioni 230 PSPF ili iweze kuwalipa.

"Kwa hiyo walimu 2,000 hawajalipwa na PSPF takribani Sh. bilioni 150 kwa sababu Serikali haijapeleka na pia walimu hawajarudishwa nyumbani baada ya kustaafu," alisema Mukoba.
Kwa mujibu wa Mukoba, hata walimu 84,000 waliopandishwa madaraja Februari na Machi mwaka huu, kati yao ni walimu 5,000 tu ndiyo waliorekebishiwa mishahara, huku wengine 78,000 wakiwa bado kurekebishiwa mishahara hiyo.


Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo