Vyeti Darasa la 7, Kidato cha Nne sasa kwa kupanda miti


Mwandishi Wetu, Iringa

January Makamba
KUANZIA mwakani kigezo cha wanafunzi  kupata cheti cha kumaliza darasa la saba na kidato cha nne ni pamoja na kuonyesha miti aliyopanda mwanafunzi huyo siku aliyoanza masomo na kuitunza vizuri hadi alipohitimu.

Kwa mujibu wa utaratibu huo mpya, anayemaliza darasa la saba anapaswa kuonyesha mti mmoja wakati kidato cha nne atapaswa awe na miti mitatu.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, January Makamba alitoa kauli hiyo aliposhiriki upandaji miti na wanafunzi wa Shule ya Msingi Mlandege iliyoko katika Kata ya Kwakilosa, Manispaa ya Iringa.

“Kuanzia mwakani kila mwanafunzi wa darasa la kwanza akiripoti shule tu atatakiwa kuja na mche wa mti na ataupanda na kuutunza kwa miaka yote saba na hatapewa cheti cha kumaliza darasa la saba kabla hajaonyesha mti wake,” alisema Makamba kwenye ziara yake mkoani hapa, akifafanua:

“Katika shule zenye maeneo madogo, miti hiyo itapandwa katika maeneo yatakayoelekezwa na Serikali za Vijiji na Mitaa. Kwa wanafunzi wa Sekondari, itakuwa hivyo hivyo lakini itakuwa miti mitatu.”

Alisema ofisi yake kuanzia mwakani itatoa maagizo kwa halmashauri zote nchini kusimamia mpango huo katika shule zote za serikali na zile za binafsi.

Alisema kila mwanafunzi wa darasa la kwanza atahitajika kufika shuleni na mche mmoja wa mti siku ya kuanza masomo ikiwa kama moja ya mahitaji ya msingi.

Kwa upande wa wanafunzi wa sekondari, alisema watapaswa kufika na miche mitatu wakati wa kuanza masomo.

Makamba amebainisha kuwa ofisi yake itatoa maelekezo kwa Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi pamoja na Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) kuwa moja ya mahitaji ya kupewa cheti cha kuhitimu ni kukabidhi miti iliyopandwa wakati mwanafunzi anafika shule kuanza masomo.

Ili apate cheti hicho, alisema mwanafunzi atahitajika kutunza na kuhudumia miti hiyo kipindi chote cha masomo.

Kutokana na hatua hiyo, alisema kuanzia Novemba 5 hadi 6, mwaka huu kutakuwa na mkutano wa wakuu wa wilaya, wakurugenzi, wenyeviti na mameya wote ili kupewa mafunzo na miongozo inayohusu mpango huo wa kuhifadhi mazingira nchini.

Katika mpango huo wa kuifanya nchi kuwa ya kijani, alisema kutakuwa na mkakati wa kulinda vyanzo vya maji.


Makamba alisema lengo la kushiriki upandaji miti pamoja na wanafunzi hao ni kutuma ujumbe kwamba uhifadhi, usimamizi na utunzaji wa mazingira ni jukumu la msingi kwa manufaa ya kizazi kijacho.

Kuhusu shule zenye uhaba wa ardhi ya kutosha kupanda miti, Makamba alisema viongozi wa serikali watakaa chini kutafuta maeneo yatakayoendelezwa kwa mpango huo.

Waziri huyo mwenye dhamana ya Mazingira amesema hili linafanyika ikiwa ni moja kati ya hatua mahsusi, stahiki na za makusudi zinazochukuliwa na Serikali katika kuendana na mabadiliko ya tabia nchi, hasa ikizingatiwa kuwa asilimia 61 ya nchi yetu ipo katika tishio la kuwa jangwa.

Waziri ametumia kifungu cha sheria ya Mazingira Sura ya 191 ya mwaka 2004 kutoa maagizo hayo ambacho kinasema “Waziri atakuwa msimamizi mkuu wa masuala ya mazingira na kwa mantiki hiyo atatoa miongozo muhimu ya sera ili kukuza, kulinda na kusimamia kiendelevu mazingira nchini Tanzania.

“Waziri anaweza kutoa miongozo ya jumla kwa wizara, idara za serikali, baraza, kamati ya taifa ya ushauri wa mazingira, jiji, manispaa, kamati ya usimamizi wa mazingira wa wilaya, wakala au asasi nyingine yoyote ya umma au binafsi, miongozo ambayo ni muhimu kwa ajili ya kutekeleza au kufanikisha yaliyoelezwa kwenye sheria hii.”

Mwisho


Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo