Scorpion aachiwa huru kwa dakika tano


Jemah Makamba

MAMIA ya watu waliofurika katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam, jana walipigwa na butwaa baada ya kushuhudia mshtakiwa wa utoboaji macho na uporaji, Salum Njewete maarufu kwa jina la Scorpion akiachiwa huru.

Tukio hilo lilitokea baada ya upande wa mashtaka mbele ya hakimu Adelf Sachore wa mahakama hiyo kuamua kuiondoa kesi hiyo katika hali ambayo sababu zake hazikuweza kufahamika mara moja.

Awali, Mwendesha Mashtaka SP Munde Kalombora aliomba mahakama kuliondoa shtaka hilo chini ya kifungu cha sheria 91(1) cha kanuni ya adhabu na hakimu Sachore kukubali akitumia kifungu hicho.

Hata hivyo, baada ya hakimu Sachore kumaliza kuondoa shtaka hilo akieleza haliwezi kuendelea tena kwenye chemba yake, Scorpion alitoka nje.

Lakini wakati watu waliofurika kusikiliza kesi hiyo wakiendelea kushangaa, polisi walimkamata tena na kumpeleka katika mahabusu ya mahakama hiyo.

Scorpion alikaa kwenye mahabusu hiyo kwa takriban takika tano, kisha alitolewa akiwa kwenye ulinzi mkali akiwa amefungwa pingu mikononi na kufikishwa tena mahakamani kwa hakimu mwingine na kusomewa upya mashtaka hayo.

Safari hii, mashtaka hayo yalisomwa mbele ya Hakimu Flora Haule.

Katika shtaka hilo jipya, mwendesha mashtaka, Chesensi Gavyole alidai mbele ya hakimu huyo kuwa Septemba 6 mwaka huu, maeneo ya Buguruni Sheli, Scorpion alifanya kosa la wizi wa kutumia silaha.

Alidai kuwa kabla ya kufanikisha wizi huo alimjeruhi kwa kumchoma kisu malalamikaji sehemu ya mabega na tumboni, kisha kumchoma macho yote mawili kwa kutumia kisu na kumuibia cheni ya fedha, kidani na pesa taslimu, vyote vikiwa na thamani ya Sh. 476,000.

Baada ya usomewa mashtaka hayo, mshtakiwa huyo alisema halitambui jina la Scorpion akidai si jina lake huku akikana mashtaka aliyosomewa.

Mwendesha mashtaka alisema upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika na Hakimu Haule alinukuu kifungu cha cha sheria namba 148 (5) (a)(i) kinachozuia watuhumiwa wa makosa kama hayo kupata dhamana na kuamua kuwa ataendelea kukaa rumande hadi Novemba 2 mwaka huu kesi hiyo itakapotajwa tena.

NJE YA MAHAKAMA

Watu walioonekana kujaa shauku ya kumjua mtuhumiwa huyo walijaa nje ya mahakama kusubiri kinachoendelea. Wingi huo wa watu uliwalazimu Polisi kutumia nguvu ya ziada kuwadhibiti.

Ndugu wa mlalamikaji akiwemo mama mzazi walifika mahakamani hapo mapema na walionekana wenye huzuni pale walipomuona mshtakiwa huyo alipofika mahakamani hapo na kushuka kwenye gari la magereza.

Hata hivyo wakati ndugu hao wa mlalakaji wakionekana kuhudhunika, ndugu wa Scorpioni walisikika wakisema kuwa hawaamini kama ndugu yao huyo anaweza kufanya unyama kama huo.

Mmoja wa wadogo wa mlalamikaji alimwambia mwandishi wa habari hii kuwa alifika mahakamani hapo ili kuona mwisho wa kesi hiyo.

“Lazima nije ni kama namwakilisha ndugu yangu ambaye sasa hawezi kufanya chochote. Hawezi hata kufuatilia kesi hiyo na kuona mwisho wake,” alisema ndugu huyo.




Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo