Serikali yatenga bilioni 70/- kununulia dawa, vifaatiba


Joyce Kasiki, Dodoma

MAKAMU wa Rais, Samia Suluhu Hassan amesema Serikali imetenga jumla ya Sh bilioni 70 za kununua dawa na vifaatiba ili kumaliza tatizo la ukosefu wa dawa nchini.

Pia  imetenga Sh bilioni 85 za kupunguza deni linalodaiwa na Bohari Kuu ya Dawa (MSD) ili Bohari hiyo itoe huduma bora ya dawa kwa wananchi.

Akifungua mkutano mkuu wa waganga wakuu wa mikoa na wilaya zote nchini jana  mjini hapa, Samia alisema dawa hizo zitakazonunuliwa zitakwenda  moja kwa moja kwenye vituo vya afya nchini.

Alisema lengo la Serikali ni kupunguza changamoto zilizo kwenye sekta ya afya, huku akiweka bayana dhamira ya Serikali ya kujenga kiwanda cha dawa mkoani Simiyu.

“Kwa mwaka huu tumepanga kwenye bajeti Sh bilioni 85 ambazo tutapunguzia deni la MSD ili iweze kutoa dawa kwa hospitali zetu,

“Lakini pia tumetenga Sh bilioni 70 kwa ajili ya kupeleka dawa vituoni, lakini ninyi mna ya kwenu, hata pale mnapokuwa na pesa mna hiari mwende kwenye maduka binafsi, lakini MSD nao wana yao, tutakaa nao tuseme nao, wahakikishe dawa zinazotakiwa zipo kwenye MSD,”alisema.

Mbali na hilo, alizungumzia suala la tiba asili na mbadala na kuitaka Wizara ya Afya, kuhakikisha inazitambua dawa hizo na kuzisajili.

“Tunapaswa tuzijue na tuzifanyie utafiti dawa za asili, tukiridhika na utafiti kwamba dawa inatibu kitu fulani, basi tuisajili, tusajili  anayeshughulikia dawa yenyewe na kuona jinsi tutakavyoiendeleza.

“Tiba asili na mbadala zina umuhimu, kama tunavyojua tuna upungufu mkubwa katika sekta ya afya hasa vijijini, zinazotusaidia ni tiba asili, naomba tuzipe umuhimu,” alisisitiza.

Mwenyekiti wa Waganga hao, Dk Sudi Leonard alisema ukosefu wa dawa na vifaa tiba kwenye baadhi ya vituo vya afya nchini unasababisha malalamiko kwa wananchi kutokana na mchakato mrefu wa upatikanaji wa dawa hizo kutoka MSD.

“Kwa sasa maombi yetu ya dawa hupatikana kwa asilimia 40 hadi 55 na zinazokosekana inatulazimu kununua nje ya MSD,” alisema Dk Leonard.

Mkutano huo ni wa siku nne ambao ulishirikisha waganga wakuu wa mikoa na wilaya na wauguzi, lengo likiwa ni kujadili masuala yahusuyo sekta ya afya zikiwamo changamoto na namna ya kuzitatua.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo