Seif amburuza Msajili wa Vyama kortini


* Apinga kumtambua Lipumba uenyekiti CUF
* AG naye ajumuishwa kwenye kesi hiyo



Grace Gurisha

BODI ya Wadhamini ya Chama cha Wananchi (CUF), imefungua kesi katika Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam na kuwasilisha maombi matatu ikiwamo kutengua barua ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini Jaji Francis Mutungi iliyotengua uamuzi wa chama hicho wa kutomtambua Profesa Ibrahim Lipumba kama mwanachama wa chama hicho.

Mbali na Jaji Mutungi na Profesa Lipumba, bodi hiyo imewashtaki pia  Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), George Masaju na wanachama wengine 11 wa chama hicho, iliodai walikiuka taratibu na sheria za chama hicho.

Akizungumza jana nje ya mahakama hiyo baada ya kufungua kesi, Wakili wa CUF, Hashim Mziray alitaja kesi hiyo kuwa ni namba 23/2016 akieleza wameifungua kwa hati ya dharura kutokana na mambo yalivyo sasa ndani ya CUF kwani hawajui hata ofisi zingine zinaendeshwaje.

“Katika maombi hayo tunaiomba mahakama mambo matatu ambayo ndiyo yanayosababisha kufukuta kwa mgogoro ndani ya CUF tukiomba yatenguliwe ili shughuli za kisiasa ziendelee,” alisema Mziray.

Alitaja jambo la kwanza kuwa ni kuiomba Mahakama itengue barua ya Msajili huyo ya Septemba 23 iliyotengua uamuzi wa CUF kumfukuza uanachama Profesa Lipumba na kumhalalisha kuwa ni mwanachama hai wa chama hicho kama mwenyekiti.

Mziray alisema suala la pili ni kuitaka Mahakama imzuie Jaji Mutungi kuingilia masuala ya Profesa Lipumba na CUF kwa sababu tayari wao wameshamfuta uanachama kwa kuwa kazi ya msajili ni kusajili vyama na si kuingilia mambo ya ndani ya vyama.

“Bodi pia inaomba mahakama hiyo itengue masuala hayo kwa sababu chama kinataka kufanya siasa, lakini hakiwezi kufanya lolote sasa kwa sababu kikwazo ni Msajili Jaji Mutungi, tunaomba azuiliwe ili mambo ya CUF yaendelee,” alisema Mziray.

Akizungumzia sababu za kufungua kesi hiyo kwa hati ya dharura, Mziray alisema wamefanya hivyo kwa kuwa kinachoendelea ni hatari, hivyo kutokana na ukweli kwamba hawawezi kufanya jambo lolote wanashindwa kudhibiti ofisi za chama, ikiwemo ofisi ya Buguruni.

“Wanachama wanashauku kubwa ya kujua nini kinaendelea na mwafaka ambao umefikiwa ndani ya chama, ndiyo maana tumefungua kwa hati hiyo ya dharura kwa sababu hivi sasa Mahakama zinasikiliza kesi kwa haraka na kutolewa uamuzi ndiyo maana wakakimbilia mahakamani,”alisema Mziray

Kaimu Naibu Mkurugenzi wa Hahari wa CUF, Mbaraka Maragande alisema anashangazwa na Mkurugenzi wa Mashataka (DPP) kwa kushindwa kufutilia vitendo vya kijinai alivyodai vilifanywa na vijana wa Profesa Lipumba.

“Ametekwa kiongozi wa CUF hakuna lolote lililofanyika la kuwakamata wahusika, lakini cha kushangaza tukio lililokuja nyuma ndiyo limefanyiwa kazi la kuwakamata vijana wetu 23 na kuwapeleka mahakamani ambao walikuwa wanatoka Zanzibar kuja kuweka ulinzi huku.

“Leo (jana) tulikwenda ofisini kwa DPP kufuatilia mashtaka tuliyoyatoa polisi, lakini hatukukuta jambo lolote linalohusiana na mashtaka yetu. Awali tulikataa kuhojiwa kwa sababu walitaka kutupa kesi nyingine tofauti, kwa hiyo ZCO na DPP hawatutendei haki katika hili Jeshi la Polisi linatakiwa lifanye kazi bila kuegemea upande wowote.

Alisema matukio hayo yalifanywa na vijana wa Lipumba Agosti 21 mwaka huu na Septemba 16 wakiwa Ubungo Plaza, jijini Dar es Salaam, lakini hadi leo hakuna hatua iliyochukuliwa.

Mgogoro ndani ya CUF umeibuka mara baada ya Lipumba kutangaza kurejea madarakani akifuta barua yake ya kujiuzulu kwenye wadhifa wake wa uenyekiti wa chama hicho aliyoiwasilisha Agosti mwaka jana.

Mgogoro huo hatimaye ulifika kwa Msajili wa Vyama vya Siasa ambaye alitoa mwongozo unaoonyesha kumtambua Lipumba kisheria, huku upande mwingine unaoongozwa na Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad ukiweka msimamo wa kutomtambua na kumfukuza uanachama.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo