Kafulila alaani Clouds kumvua kipaza-sauti


Mwandishi Wetu

ALIYEKUWA Mbunge wa Kigoma Kusini na Mkuu wa Idara ya Habari na Uenezi wa Chama cha NCCR-Mageuzi, David Kafulila amesema amepatwa na mfadhaiko kwa kitendo cha kuahirishwa kwa mahojiano katika Kituo cha Televisheni cha Clouds kupitia kipindi cha 360.

Kafulila alisema amepatwa na mfadhaiko mkubwa kwa mahojiano hayo ambayo yalikuwa yanahusu kujadili mambo mbalimbali ya nchi na kwamba kitendo hicho kina mkono wa viongozi wa Serikali wakubwa.

“Inasikitisha kuona kipindi kimetangazwa tangu jana (juzi) na nimefika na kuvaa kipaza sauti halafu unaambiwa kuna agizo kutoka kwa mkurugenzi kipindi kisirushwe nimefadhaika sana sana,” alisema.

“Hadi kipindi cha magazeti saa mbili asubuhi nilikuwa studio na mtangazaji akatangaza kuwa  baada ya magazeti Kafulila ataingia kujadilia masuala mbalimbali yanayoendelea nchini.

Nikiwa studio tayari nimevaa kipaza sauti, ikaombwa radhi kwamba kuna maelekezo kutoka kwa mkurugenzi kuwa kipindi kisirushwe,” aliongeza

Kafulila alisema anadhani kulikuwa na maelekezo ya ziada nje ya mfumo wa Clouds Tv kwa sababu haamini kama tangazo limerushwa kutwa nzima jana (juzi) na jana asubuhi bila mkurugenzi huyo kujua.

Mbunge huyo wa zamani alihoji iwapo mkurugenzi huyo hakujua bado vipindi ni suala la wataalamu wa utangazaji kuliko mmiliki na kwamba hajajua hofu yao ilikuwa wapi.

Mkuu huyo wa idara alisema kinachoondelea kwa sasa kwa mtazamo wake ni kuminya uhuru wa vyombo vya habari, huku akibainisha kuwa Sheria ya habari inayokwenda kupitishwa bunge lijalo, vyombo vyote vitakuwa chini ya ulinzi wa dola.

“Binafsi sikutarajia siku moja kukutwa na hali hiyo sikujua kama siku moja Tanzania itafika hatua hii nilijisikia vibaya kuvuliwa kipaza sauti nikiwa tayari kwa mjadala, lakini nilijua tatizo ni zaidi ya watangazaji,” alisema.

Aidha, alisema alikuwa amejipanga kuelezea tatizo la mwenendo wa uchumi kuanzia namna Serikali iliyorithi uchumi mbovu na haionekani kutambua hilo na kujizatiti na badala yake hali imezidi kuwa mbaya.

Alisema pia alitaka kuzungumzia kwa mapana anguko la sekta ya fedha na sekta binafsi na mazingira ya biashara na uwekezaji kwa ujumla na namna athari yake inavojitokeza kwenye kupunguza uwezo wa serikali kutoa huduma kama elimu, afya,  kwa mujibu wa repoti mbalimbali za tafiti.

“Nilitaka kuhitimisha kwa kuzungumzia mwenendo wa vita ya ufisadi, hatua zinazochukuliwa na maoni juu ya nini bado hakijafanyika,” alisema.

Aidha, kwa upande mwingine Chama cha NCCR-Mageuzi kimetoa taarifa ya kulani kitendo cha Kafulila kutofanya mahojiano hayo na kuwataka Watanzania kutambua kuwa kuna kazi kubwa ya kulinda demokrasia na utawala wa sheria.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo