PM amwagiza Waziri kukarabati Bodi ya Korosho


Mwandishi Wetu

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemwagiza Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk Charles Tizeba kuifanyia marekebisho makubwa Bodi ya Korosho na Menejimenti yake,  baada ya kushindwa kusimamia zao hilo ipasavyo.

Amesema Serikali itafanya mapitio ya bodi zote za mazao ya biashara na imeanza na korosho baadaye pamba, tumbaku, kahawa, katani na chai. Katika tathmini na mapitio hayo, bodi itakayobainika kushindwa kutekeleza majukumu yake itavunjwa.

Waziri Mkuu alitoa agizo hilo juzi alipohutubia wananchi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja cha Sokoine wilayani Nachingwea mkoani Lindi.

Aliishangaa bodi hiyo kuacha kutekeleza majukumu yake na kuingilia minada ya korosho na kuzuia baadhi ya wafanyabiashara kununua zao hilo hali inayoashiria kuwapo watu waliopangwa kununua bila ya utaratibu.

“Bodi leo wamejipa jukumu la kusimamia minada! Si kazi yao ni ya chama kikuu, korosho inalimwa kuanzia Ruvuma hadi Tanga, mtasimamia minada mingapi? Viachieni vyama vikuu.

“Vyama vikuu vikiharibu walalamikaji waje kwenu kama sehemu ya rufaa. Ninyi mnasimamia minada mnaharibu, walalamikaji watakwenda kwa nani?  Kwa nini mng’ang’anie kwenda kwenye minada?” Alihoji Waziri Mkuu.

Waziri Mkuu alisema Ijumaa bodi hiyo ilisitisha mnada wa korosho Lindi kwa sababu wanunuzi hawakuweka dhamana ya mauzo na alishatoa maagizo ya kutaka wanunuzi wasiruhusiwe kununua hadi waweke asilimia 25 ya malipo.

Alisema maagizo hayo aliyatoa tangu Aprili ila  watendaji wa bodi hiyo hawakuyafanyia kazi kwa wakati na badala yake walizuia wafanyabiashara waliotaka kununua korosho Lindi kwa madai ya kutokuwa na bondi huku wakiruhusu wa Mtwara.

“Kama kule walinunua bila bondi kwa nini wasiruhusu na Lindi wakanunua bila bondi ili nijue kwamba mliamua kugoma kutekeleza maelekezo ya Serikali? Au hamkumtaka aliyeshinda  nyie  mlikuwa mnamtaka nani? Nitashughulika nanyi,” alisisitiza.

Aliongeza: “Nimesema tukitoa maelekezo lazima yatekelezwe na atakayeshindwa hatufai, Mheshimiwa Mbunge umelalamika juu ya Bodi, hawa ndio wabeba maelekezo, hatujawahi kuona bodi ya korosho ikienda vijijini kuzungumza na vyama vikuu hata mara moja.”

Akizungumzia suala la wakulima kulazimishwa kufungua akaunti  za kupitishia malipo yao alisema wasiwalazimishe. “Waelimisheni wakulima umuhimu wa kufungua akaunti, lakini si kwa kuwalazimisha wote wawe na akaunti hadi yule mwenye kilo tano…na akaunti yenyewe inafunguliwa kwa Sh 100,000,” alisema.

Alisema: “Wanashindwa kutekeleza niliyowaagiza, halafu wanasingizia utendaji wao mbovu kuwa ndio maagizo yangu, niliwaagiza wapi?” Alihoji na kuongeza: “Yapo makundi yanafanya mambo yanavyotaka halafu yakiwazidi mambo wanasingizia viongozi wa juu na ndio wale wanaosema kila kitu nimeagizwa kutoka juu, juu wapi?

“Lazima tuendelee kudhibiti nidhamu ya vyombo tunavyounda kwa ajili ya kuhudumia wananchi. Tutaendelea kusimamia nidhamu kwa taasisi zinazohudumia wakulima nchi nzima,” alisisitiza.

Wakati huo huo, Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Godfrey Zambi alimkabidhi Waziri Mkuu msaada wa Sh milioni 16.3 pamoja na nguo kwa ajili ya kusaidia wananchi walioathirika na tetemeko la ardhi mkoani Kagera.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo