Lukuvi aagiza chuo kitumike kurasimisha makazi


Peter Kimath, Morogoro

WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi ameagiza Chuo cha Ardhi mjini hapa kitumike katika urasimishaji wa makazi, kutokana na kukosa wataalamu wa kutosha kukamilisha kazi hiyo.
  
Waziri Lukuvi alisema jana kuwa Serikali haina uwezo wa kuajiri wataalamu wa kupima na kupanga makazi hayo na waliopo hawatoshelezi, hivyo ili kuondokana na makazi ambayo hayajapimwa ni vema wataalamu wa chuo hicho wakatumika.

Alisema ili kuchukua muda mfupi ipo haja ya kutumia chuo hicho   na kampuni zinazotambulika, zilizosajiliwa  na wizara hiyo kwa upimaji wa ardhi na makazi.

Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro, John Mgalula alisema wanatarajia kupata mkopo wa Sh milioni 100 kutoka benki ya CRDB, fedha zinazotarajiwa kurasimisha viwanja 1,000 kwa majaribio.

Kauli hiyo ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro ilisababisha Waziri Lukuvi kuitaka Manispaa kuacha kusubiri mikopo na badala yake itumie mbinu mbadala ya kuzungumza na kampuni na chuo hicho cha ardhi ili kukubaliana kupima.

Mkuu wa Chuo, Desderius Kimbe alisema chuo kiko tayari kufanya kazi hizo kutokana na kwamba wana wataalamu hao ambao wanaweza kufanya kazi hizo, pia wana vitendea kazi vya kutosha kufanikisha kazi hiyo.

Mratibu wa Urasimishaji Ardhi, Adolph Milunga alisema mbali na  kuwa  chuo pekee kinachofundisha wataalamu wa upimaji ardhi katika  ngazi ya Shahada na Stashahada, chuo hicho pia kinafanya   upimaji ardhi na kutoa ushauri juu ya masuala ya ardhi.

Milunga alishauri wananchi wa Morogoro, ili kupunguza gharama  wajiunge kwenye vikundi katika maeneo yao badala ya kuomba kupimiwa mmoja mmoja.


Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo